Waziri mkuu wa zamani Algeria afikishwa kizimbani kwa tuhuma za ufisadi
Waziri mkuu wa zamani wa Algeria Ahmed Ouyahia amefikishwa mahakamani mjini Algiers Jumapili kusailiwa kuhusu tuhuma za ufisadi unaohusu mshirika mmoja wa Algeria na shirika la Volkswagen la Ujerumani.
Hii ni mara ya pili kwa Ouyahia kufikishwa mahakamani tokea Mahakama ya Kilele iamuru akamatwe wiki iliyopita kwa ajili ya uchunguzi kuhusu kashfa ya ufisadi.
Wakati huo huo waziri wa zamani wa Fedha Algeria Karim Djoudi naye pia alifikishwa mbele ya Mahakama ya Kilele Jumapili kujibu maswali kuhusu tuhuma za ufisadi.
Bado hajafunguliwa kesi lakini anajiunga na maafisa kadhaa wa ngazi za juu katika utawala wa rais wa zamani wa Rais Abdelaziz Bouteflika ambao wanachunguzwa kuhusu ufisadi. Waziri wa zamani wa biashara Amara Benyounes naye pia anatazamiwa kufunguliwa kesi ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.
Mahakama ya Kilele ya Algeria inachunguza kashfa hizo za ufisadi huku maandamano ya wananchi yakiendelea nchini humo hata baada ya Bouteflika kujiuzulu wakitaka wote wanaofungamana naye waondoke na waliohusika na ufisadi wafikishwe kizimbani.
Abdelaziz Bouteflika alilazimika kujiuzulu kama rais wa Algeria mwezi Aprili kufuatia maandamano makubwa ya wananchi miezi miwili iliyopita baada ya kutawala kwa muda wa miaka 20.
Waalgeria sasa wanataka mabadiliko kamili ya kisiasa huku wakisisitiza kuwa wale wote wanaofungamana na utawala wa Bouteflika wanapaswa kuachia ngazi na waliohusika na uhalifu wafikishwe kizimbani.