Makumi ya watu waaga dunia kwenye mgodi Kongo DR + Sauti
Makumi ya wachimba migodi wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa shaba nyekundu na kobalti huko kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Duru za habari zinasema watu 43 wameaga dunia katika maporomoko hayo yaliyotokea kwenye mgodi huo unaosimamiwa na kampuni ya Glencore yenye makao makuu yake mjini Baar nchini Uswisi.
Kwa mujibu wa Joseph Yav Katshung, afisa mkuu katika Ofisi ya Gavana wa mkoa wa Lualaba, ajali hiyo ya jana ilitokea katika Mgodi wa Kamoto Copper Company (KCC) karibu na mpaka wa nchi hiyo na Zambia. Amesema wanahofia kuwa kuna miili mingine ingali imefukiwa kwenye maporomoko hayo.
Gavana wa mkoa huo, Richard Muyej amesema askari jeshi wa DRC wametumwa kwenye mgodi huo, kwa ajili ya kusaka maiti zilizofukiwa sambamba na kulinda usalama wa mgodi huo.
Awali vyombo vya habari vilikuwa vimeripoti kuwa ni watu 16 tu wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo. Hii sio mara ya kwanza kwa wachimba migodi nchini DRC kupoteza maisha yao.
Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini hususan ya dhahabu na almasi yanayochimbwa Kongo DR husafirishwa kimagendo katika nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na kisha Dubai huko Imarati, kabla ya kupelekwa katika nchi za Ulaya.
Maelezo zaidi yamo katika ripoti iliyoambatana na habari hii iliyoletwa kwenu na mwandishi wetu Mossi Mwasi.