Mahakama yaakhirisha kutoa hukumu dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54922-mahakama_yaakhirisha_kutoa_hukumu_dhidi_ya_sheikh_ibrahim_zakzaky
Mahakama Kuu katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria imeakhirisha kutoa hukumu ya kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 22, 2019 03:29 UTC
  • Mahakama yaakhirisha kutoa hukumu dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky

Mahakama Kuu katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria imeakhirisha kutoa hukumu ya kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Duru za karibu na mahakama hiyo zimeeleza kwamba, mahakama hiyo imewajulisha mawakili wa Sheikh Zakzaky kwamba, hukumu ya kesi ya mteja wao itatolewa siku kumi zijazo.

Mahakama Kuu ya Kaduna imeakhirisha kutoa hukumu dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, katika hali ambayo hali ya kiafya ya mwanaharakati huyo inaripoti kuzidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Aidha tangazo la Mahakama Kuu ya Kaduna linatolewa huku, maandamano ya kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky yakiendelea kushuhudiwa ndani na nje ya Nigeria.

Waislamu wakiandamana nchini Nigeria kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Mwaka 2015, jeshi la Nigeria lilivamia na kushambulia mkusanyiko wa Waislamu katika Husseiniya ya Zaria kwenye jimbo la Kano na kuua shahidi kwa umati karibu Waislamu elfu moja akiwemo mtoto wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Sheikh Zakzaky mwenyewe na mkewe walipigwa risasi na tangu wakati huo wanashikiliwa katika korokoro za serikali ya Rais Muhammadu Buhari ambayo inaendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kumwachilia huru mwanachuoni huyo.

Ripoti mbalimbali za uhakika zinasema kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya na hata damu yake imegunduliwa kuwa na chembe chembe za risasi kutokana na mateso anayopewa huku hali yake na mkewe ikizidi kuwa mbaya, siku baada ya siku.