Wasomi 52 wamtaka Guterres aingilie kati kadhia ya Sheikh Zakzaky
Wasomi na wanafikra 52 wamemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asaidie jitihada za kutaka kuachiwa huru mara moja Sheikh Ibrahim Zakzaky huko Nigeria kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kituo cha habari cha Global Research kimeripoti kuwa, wasomi mashuhuri 52 na wanaharakati wamemwandikia barua ya wazi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakimtaka achukue hatua za haraka za kuhakikisha kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mwewe Malam Zeenat, wanapewa matibabu.
Barua hiyo inasema kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na mkewe ni mbaya sana kutokana na majeraha yaliyosababishwa na mateso waliyopewa na maafisa wa serikali ya Nigeria na imemtaka Katibu Mkuu wa UN kuishinikiza serikali ya Abuja ili iruhusu Sheikh Zakzaky na mkewe wapelekwe nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Sehemu moja ya barua ya wasomi hao inasema kuwa: Kuendelea kushikiliwa kwa muda mrefu Sheikh Zakzaky katika korokoro za Nigeria na kuzuiwa kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu ni doa jeusi katika historia ya serikali ya Nigeria. Wasomi hao wamesisitiza kuwa: Hatua ya Rais wa Nigeria ya kutoruhusu Sheikh Zakzaky na mkewe wapatiwe matibabu ni kielelezo zaidi cha ukatili na dhulma za serikali yake.
Mwaka 2015, jeshi la Nigeria lilivamia na kushambulia mkusanyiko wa Waislamu katika Husseiniyah ya Baqiyatullah huko Zaria kwenye jimbo la Kano na kuua shahidi karibu Waislamu elfu moja.
Sheikh Zakzaky mwenyewe na mkewe walipigwa risasi na tangu wakati huo wanashikiliwa katika korokoro za serikali ya Rais Muhammadu Buhari ambayo inaendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kumwachilia huru mwanachuoni huyo.