Guterres aombwa kufuatilia hali ya Sheikh Zakzaky ili apatiwe matibabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54969-guterres_aombwa_kufuatilia_hali_ya_sheikh_zakzaky_ili_apatiwe_matibabu
Wasomi na wanafikra 52 wamemwandikia barua Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakimtaka asaidie jitihada za kuwaondoa huko Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe Malam Zeenat ili waweze kupatiwa matibabu nje ya nchi haraka iwezekanavyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2019 22:08 UTC
  • Guterres aombwa kufuatilia hali ya Sheikh Zakzaky ili apatiwe matibabu

Wasomi na wanafikra 52 wamemwandikia barua Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakimtaka asaidie jitihada za kuwaondoa huko Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe Malam Zeenat ili waweze kupatiwa matibabu nje ya nchi haraka iwezekanavyo.

Hiyo ni kufuatia kuzidi kuwa mbaya hali ya kimwili na kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Barua hiyo inasema kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na mkewe ni mbaya sana kutokana na majeraha yaliyosababishwa na mateso waliyopewa na maafisa wa serikali ya Nigeria na imemtaka Katibu Mkuu wa UN kuishinikiza serikali ya Abuja ili iruhusu Sheikh Zakzaky na mkewe wapelekwe nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. 

Katika wiki za karibuni duru za habari zilizo karibu na familia ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walitangaza kuwa hali ya kiafya na kimwili ya Sheikh Zakzaky ni mbaya sana na zimetoa wito wa kuachiwa huru haraka mwanazuoni huyo ili apatiwe matibabu. Hata hivyo serikali ya Nigeria inaendelea kukaidi wito huo. Kwa kadiri kwamba Idara ya Mahakama ya Nigeria tarehe 21 mwezi Julai pia  kwa mara nyingine iliakhirisha kutoa uamuzi kuhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky baada ya kufanyika majadiliano na mazungumzo kati ya mawakili na msomi huyo na waendesha mashtaka katika Mahakama Kuu ya Jimbo la Kaduna. 

Kushtadi maradhi ya Sheikh  Zakzaky na kupewa sumu akiwa jela kumezidi kuwatia wasiwasi Waislamu wa Nigeria. Kwa msingi huo, katika wiki za hivi karibuni wananchi wa Nigeria wamezidisha maandamano wakitaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo. Hata hivyo maandamano hayo yanakabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa askari usalama wa Nigeria kiasi kwamba hadi kufikia sasa watu zaidi ya 11 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika ukandamizaji huo wa askari polisi wa Nigeria dhidi ya maandamano ya kumuunga mkono Sheikh Zakzaky.  

Wakazi wa Abuja wakiandamana kutaka kuachiwa huru Sheikh Zakzaky

Kitendo cha kukaidi kumuachia huru Sheikh Zakzaky na kuzuia matibabu yake kinajiri katika hali ambayo Mahakama Kuu ya NIgeria mwezi Disemba mwaka 2016 ilitoa hukumu ya kufutiwa mashtaka na kuachiwa huru Zakzaky. mahakama hiyo pia iliagiza msomi huyo mkewe walipwe fidia. Hata hivyo si tu kuwa hukumu hiyo haijatekelezwa bali hadi hadi sasa viongozi wa Nigeria hawajaafiki kumuachia huru mwanazuoni huyo licha ya kusumbulwia na maradhi. Kutoachiwa huru Sheikh Zakzaky katika hali ngumu ya sasa na kimya cha taasisi za kimataifa mkabala ya utendaji wa serikali ya Nigeria na kukiukwa haki za kibinadamu za Sheikh Ibrahim Zakzaky yote hayo yamewakasirisha sana Waislamu na wapigania ukombozi duniani. 

Sayyid Abbas Mousavi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria hali inayozidi kua mbaya ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na kueleza kuwa: Inatazamiwa kuwa viongozi husika wa Nigeria watachukua hatua haraka iwezekanavyo na kwa wakati mwafaka kumwachia huru na kumpeleka Sheikh Ibrahim Zakzaky nje ya nchi kwa ajili ya matibabu anayohitajia. 

Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
 

Serikali ya Nigeria inayoathiriwa na mashinikizo ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Saud Arabia, inaendelea kukaidi uamuzi wa kuachiwa huru msomi huyo wa Kiislamu na kumtendea haki zake za kisheria. Katika miaka ya karibuni si tu kuwa haki za Waislamu nchini humo zimekiukwa bali ukandamizaji dhidi yao pia umeongezeka katika fremu ya matakwa ya Marekani na waitifaki wake; na kushindwa kuachiwa huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya  Nigeria kunaweza kunatathminiwa katika uwanja huo. 

Shaib Muhammad mwakilishi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameeleza kuwa maadui wana lengo la kuchafua taswira ya harakati hiyo na kwamba kunashuhudiwa mkono wa utawala wa Aal Saud na Wazayuni katika kutiwa mbaroni Sheikh Zakzaky.  

Waislamu wa Nigeria wanaendelea kufanya juhudi na kila wawezalo ili kuhakikisha kwamba Sheikh Zakzaky na mkewe wanaachiwa huru na kuhusiana na suala hilo wamewatolea wito Waislamu wote na wapigania ukombozi duniani kushiriki katika jitihada hizo. Wakati huo huo  inaonekana kuwa viongozi wa Nigeria wanakabiliwa na mtihani mgumu ambao ni amma kumuachia huru Sheikh Zakzaky na kumpatia matibabu au kuendelea kukaa kimya na kuwashinikiza Waislamu.  

Masoud Shajare Mkuu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu anatahadharisha kuhusu suala hilo kwamba: Baadhi ya madola ya kigeni yamegharimika pakubwa na hayataka kuona Sheikh huyo akibaki hai."