WHO: Hakuna kesi mpya za Ebola katika mji wa Goma
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa limetoa chanjo ya Ebola kwa watu zaidi ya 1,300 ambao waliambukizwa virusi vya ugonjwa huo katika mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mlipuko wa homa ya Ebola uliodumu kwa mwaka mmoja mashariki mwa Kongo umeuwa watu 1,800 hadi sasa; idadi ambayo inatajwa kushika nafasi ya pili kwa ukubwa. Wakati huo huo jitihada za kuangamiza virusi hatari vya homa hiyo zimekuwa zikikwamishwa na mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha na wahalifu wengine. Goma ambao ni mji unaopakana na ziwa wenye jamii ya watu karibu milioni mbili ambapo pia unapakana na Rwanda umekuwa katika hali kubwa ya tahadhari wiki iliyopita baada ya mchimba madini ya dhahabu mwenye familia kubwa kuwaambukiza homa ya Ebola watu kadhaa kabla ya yeye kufariki dunia.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani imeeleza kuwa zoezi la utoaji chanjo linaloendelea sasa limefikia kiwango cha asilimia 98. Aidha hakuna kesi mpya za maambukizo ya Ebola zilizothibitishwa huko Goma tangu WHO iwasilishe ripoti yake ya mwisho tarehe pili mwezi huu.
Wakati huo huo jana Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Dunaini (WHO) lilitangaza kuwa kwa wastani watu 86 wanaambukizwa ugonjwa wa Ebola kila wiki nchini Jamhuri ya Kdemokrasia ya Kongo, katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.