WHO: Dawa mbili zilizoko kwenye majaribio zimeonyesha uwezekano mkubwa kutibu Ebola
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kkuwa, Dawa mbili mpya zinazojaribiwa kwa wagonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeonyesha kuwa, zina uwezo mkubwa wa kutibu maradhi hayo.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza kwamba, zaidi ya asilimia 90 ya watu wenye Ebola wanaweza kupona ikiwa watapatiwa matibabu ndani ya siku tatu tangu kuanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kwamba, matokeo haya yanaridhisha kwa kiasi kikubwa na jopo huru la kufuatilia majaribio ya dawa hizo limeshauri kufikiwa haraka natija ya mwisho ya majaribio hayo ya kutibu maradhi ya Ebola.
Kutokana na dawa hizo mbili kuonyesha uwezekano mkubwa wa kutibu virusi vya ugonjwa wa Ebola, imeeleza kuwa, kuanzia sasa wagonjwa wote wanaougua maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watatibiwa kwa dawa hizo mbili.
Hadi tarehe 6 mwezi huu wa Agosti, jumla ya visa 2,781 vimeripotiwa tangu kulipuka kwa ugonjwa huo Kivu Kaskazini mwezi Agosti mwaka jana na kati ya visa hivyo, wagonjwa 1,866 waliothibitishwa kuambukizwa maradhi hayo wamefariki dunia.
Ikumbukwe kuwa, mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.