Njama ya serikali ya Nigeria; safari ya kitiba ya Sheikh Zakzaky yakatizwa
Katika hali ambayo Waislamu wa Nigeria walikuwa na matumaini makubwa ya kutibiwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakayi ya Kiislamu ya Nigeria huko India, serikali ya Niigeria imetoa mashinikizo na kumlazimu sheikh huyo na mkewe kurea mjini Abuja.
Sheikh Zakzaky na mkewe ambao wamekuwa kizuizini kwa muda unaokaribia miaka minne wamepitia mateso makali na kupata magonjwa tofauti yanayohatarisha maisha yao. Katika miezi kadhaa iliyopita na kufuatia kuongezeka kwa maradhi ya Sheikh Zakzaky, Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kuishinikiza serikali imwachilie ili apate matibabu yanayofaa. Maandamano na mikusanyiko ya Waislamu na ufuatiliaji wa kimataifa ukiwemo ule uliofanywa na Antonio Guterres, katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na viongozi wengine wa kimataifa hatimaye uliilazimisha mahakama kuu ya jimbo la Kaduna kumruhusu Sheikh Zakzaky atibiwe nchini India.
Pamoja na kuwa hukumu ya mahakama hiyo iliwafurahisha Waislamu wa Nigeria lakini wengi walikuwa na wasiwasi kuhusiana na namna hukumu hiyo ingetekelezwa kwa kutilia maanani kwamba serikali ya Nigeria na mashirika ya kijasusi ya nchi hiyo yanadhibitiwa na Marekani, utawala haramu wa Israel na Saudia ambazo zinapinga shughuli za Waislamu nchini Nigeria na zinatoa mashinikizo ya kila aina dhidi yao, ili kufikia malengo yao ya kibeberu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Professor Dahiru Yahya wa Chuo Kikuu cha Bayero nchini Nigeria anasema: Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni zinashirikiana kwa karibu na serikali ya Nigeria. Udhamini wa pesa na idiolojia umekabidhiwa Saudia nao utawala wa Israel umepewa jukumu la kupanga mikakati, mauaji na kupora mali za Mashia wa Nigeria. Maudhui hii ya Wazayuni na Mawahabi kushirikiana dhidi ya Waislamu iko wazi na wala suala hilo halina shaka yoyote.
Licha ya shaka yote iliyokuwepo, hatimaye Seikh Zakzaky na mkewe wiki hii waliruhusiwa na mahakama kwenda kutibiwa nchini India huku wakiwa wamezingirwa na askari usalama. Pamoja na hayo mara tu walipowasili katika uwanja wa ndege wa New Delhi walizuiwa na maafisa wa India kwenda kwenye hospitali aliyokuwa ameichagua Sheikh Zakzaky ili atibiwe na madaktari aliowachagua yeye mwenyewe. Mara tu baada ya kuwasili, walikutana na timu ngeni kabisa ya madaktari waliokuwa hawawatambui. Kuhusiana na suala hilo, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilitangaza kwamba baadhi ya maafisa wa serikali ya Abuja walikuwa wanashirikiana na wenzao wa India ili kuvuruga mkondo wa matibabu ya sheikh huyo.
Kwa muda wa wiki moja aliyokuwa India, Sheikh Zakzaky hakupata matibabu yoyote bali alikuwa amezingirwa na kufuatiliwa kwa karibu na makachero wa Nigeria.
Sheikh alitangaza kupitia ujumbe wa video kwamba serikali ya Nigeria ilikuwa imeipa serikali ya India habari zisizo sahihi kuhusiana na kiongozi huyo na vilevile kuzuia mwenendo wa matibabu yake.
Kutokuwepo suhula, vifaa visivyofaa vya matibabu, kutokuwepo madaktari wa kuaminika, kuzuiliwa hospitalini na kisha mashinikizo ya serikali ya Nigeria ya kuitaka India imfukuze kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, ni mambo yaliyomlazimisha Sheikh Zakzaky kuchukua uamuzi wa kurejea nyumbani mjini Abuja.
Akizungumzia suala hilo, Masoud Shajareh, mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu za Kiislamu kilicho na makao makuu yake mjini London anasema: Serikali ya Nigeria inatumia kila mbinu kumuua Sheikh Zakzaky na kuangamiza harakati yake ya Kiislamu ili kuandaa uwanja wa kurejea ubeberu wa Magharibi barani Afrika.
Hata kama serikali ya Nigeria kwa ushirikiano wa Marekani na washirika wake inatumia kila mbinu kujaribu kumfuta Sheikh Zakzaky ili kupunguza uungaji mkono na ufuasi mkubwa alionao nchini humo, lakini Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na Waislamu wa nchi hiyo wanasisitiza juu ya kiongozi huyo mashuhuri kupewa matibabu ya dharura na kuendelea kuimarishwa shughuli za harakati hiyo nchini humo. Ibrahim Musa, Msemaji wa Harakati ya Nigeria anasema: Harakati ya Kiislamu ndio nguzo pekee iliyo imara barani Afrika.