Juhudi za Niger na Nigeria za kukabiliana na makundi ya wabeba silaha
(last modified Mon, 09 Sep 2019 07:27:27 GMT )
Sep 09, 2019 07:27 UTC
  • Juhudi za Niger na Nigeria za kukabiliana na makundi ya wabeba silaha

Viongozi wa majimbo ya mpakani ya Niger na Nigeria wamefanya vikao vya pamoja kwa madhumuni ya kukabiliana na vitendo vya mabavu vinavyotekelezwa na makundi ya wabeba silaha.

Jana Jumapili magavana wa majimbo manne yaliyoko katika mpaka wa pamoja wa nchi mbili hizo walitoa taarifa ya pamoja katika mji wa Maradi, kusini mwa Niger, wakisisitiza azma yao ya kupambana na makundi ya wabeba silaha katika mpaka huo na vilevile kuongeza juhudi za kuzuia vitendo vya makundi hayo kupitia kuimarishwa usalama.

Washiriki wa kikao hicho wamechunguza hali ya usalama katika maeneo ya mpaka ya Maradi nchini Niger na katika majimbo ya Katsina, Sokoto na Zamfara yaliyoko kaskazini mwa Nigeria na kukiri kuongezeka vitendo vya ubebaji silaha, zana za kijeshi na ulanguzi wa madawa ya kulevya katika maeneo hayo.

Moja ya mashambulio ya Boko Haram nchini Niger

Tangu mwaka uliopita, Niger imeimarisha usalama katika mpaka wake na Nigeria kwa lengo la kukabiliana na  makundi ya wabeba silaha ambayo yamepelekea wimbi kubwa la raia wa Nigeria kuhamia katika eneo la Maradi.

Tokea mwanzoni mwa mwezi Januari hadi tarehe 31 mwezi uliopita wa Agosti, viongozi wa Maradi wametoa taarifa za kuuawa watu 31, kujeruhiwa 34 na wengine 92 wakazi wa eneo hilo kutekwa nyara. Vilevile wamesema wabeba silaha katika eneo hilo wameweza kuiba mifugo zaidi ya elfu 3 katika kesi 81 za mashambulo ya silaha.

Tags