Kuanza tena maandamano ya wananchi huko Misri
(last modified Sun, 29 Sep 2019 07:10:24 GMT )
Sep 29, 2019 07:10 UTC
  • Kuanza tena maandamano ya wananchi huko Misri

Wananchi wa Misri kwa mara nyingine wamemiminika mitaani kulalamikia matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii wanayokabiliana nayo na kutaka kuondoka madarakani rais wa nchi hiyo Abdel Fattah al Sisi baada ya kupita miaka 8 ya vuguvufu la harakati ya wananchi wa Misri lililopelekea kung'olewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

Abdel Fattah al Sisi ambaye aliingia madarakani huko Misri mwaka 2014 baada ya kumpindua Muhammad Morsi Rais halali wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia; amekuwa akitekeleza siasa za ukandamizaji na za mabavu dhidi ya wapinzani na maandamano ya wananchi; kiasi kwamba aghalabu ya vyama vya kisiasa vya Misri vinalalamikia utendaji wa rais huyo katika uga wa kisiasa. Utendaji wa Rais al Sisi katika sekta ya kiuchumi pia hauridhiwi na wananchi. Aidha kufichuliwa ufisadi mkubwa wa Rais al Sisi na baadhi ya viongozi wengine wa serikali kumezidisha hasira na ghadhabu za wananchi wa Misri dhidi yake. Kuhusiana na suala hilo, hata kama maandamano ya wananchi yanaendelea huko Misri kwa muda sasa katika sura tofauti, lakini kushtadi ukandamizaji na kutiwa mbaroni wapinzani, kuendelea kamatakamata kiholela na kutolewa hukumu nyingi za kunyongwa na vifungo vya maisha jela, kuchapishwa ripoti kuhusu hali mbaya ya wafungwa waliopo jela, vifo vyenye kutia shaka vya baadhi ya wanasiasa kama hayati Muhammad Morsi na mwanawe wa kiume, yote hayo yamezidisha malalamiko na upinzani dhidi ya al Sisi. 

Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri 
 

Katika upande mwingine, hatua ya Mohammed Ali tajiri Mmisri ambaye yuko uhamishoni nchini Uhispania ya kuweka wazi ufisadi wa kisiasa na kiuchumi wa al Sisi imewapelekea raia wa Misri hadi elfu kumi kuandamana nchini humo siku kadhaa zilizopita katika miji mbalimbali wakitaka kujiuzulu al Sisi. Mohammed Ali ametuma jumbe kwa njia ya video akibainisha kuwa, alikuwa mkandarasi katika jeshi la Misri kwa muda wa miaka 15 na kwamba alimjengea al Sisi jumba la kifahari katika kituo cha kijeshi nchini humo. Ameongeza kuwa, kuna ufisadi mkubwa wa kiuchumi katika safu ya uongozi serikalini huko Misri; ambao umempelekea kupoteza mamilioni ya dola. Kitendo cha Mohammed Ali kufichua ufisadi mkubwa unaofanywa na viongozi wa Misri kimevifanya baadhi ya vyama vya kisiasa nchini humo pia kumuunga mkono. Chama cha uhuru cha Misri kimeashiria gharama kubwa zilizotumiwa na serikali ya Misi katika kujenga ikulu za rais katika hali ambayo wananchi wanakabiliwa na umaskini na kukemea hatua hiyo. 

Wakati huo huo kuongezeka maandamano kumezidisha pia hali ya machafuko na kamatakamata dhidi ya wapinzani wa al Sisi; kwa kadiri kwamba kwa mujibu wa ripoti za wanaharakati wa haki za binadamu huko Misri hadi sasa mamia ya waandamanaji wametiwa nguvuni katika miji mbalimbali nchini humo na kufungwa jela. 

Maandamano ya wananchi katika mji wa Suez nchini Misri dhidi ya Rais al Sisi

 

Harakati ya Mapinduzi ya Kisoshalisti imeandika kuwa: Kupinduliwa madarakani al Sisi si ndoto tena isiyoweza kutimia bali inakaribia; na wananchi wa Misri hawawezi tena kustahimili ufisadi na udikteta. Wananchi hao wanataka utawala adilifu, wa kizalendo na wa kiraia.  

Maandamano makubwa ya juzi Septemba 27 huko Misri yaliyofanyika chini ya shaari ya "Ijumaa ya Ukombozi na Mapinduzi ya Wananchi" na kuenea hadi medani ya At- Tahrir ambayo ni nembo ya kuanza harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Misri mwaka 2011, yanaweza kuwa mwanzo wa awamu mpya ya kisiasa nchini humo. Inaonekana kuwa, wananchi wa Misri wamefungua ukurasa mwingine katika historia ya nchi hiyo na kufuatilia malengo kama ya kuleta uadilifu, demokrasia, uhuru wa kisiasa na kiraia na kuboreshwa hali ya kiuchumi. Kuhusiana na suala hilo wananchi hao wanaona kuwa, kung'olewa madarakani al Sisi ni ngazi ya awali ya kuanza mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini humo. 

Tags