Mripuko wa homa ya manjano waua watu 16 nchini Nigeria
Mripuko wa homa ya manjano nchini Nigeria umesababisha vifo vya watu 16 katika jimbo la Bauchi, kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Rilwanu Mohammed, afisa wa afya mjini Bauchi amesema idadi hiyo imeongeka kutoka ile ya watu saba iliyoripotiwa mapema mwezi huu, kutokana na wakazi kukataa kupewa chanjo.
Amesema kesi 119 za ugonjwa zimerekodiwa katika jimbo hilo, na kwamba 20 kati yazo zimeweza kuthibitishwa kufikia sasa baada ya vipimo kuchukuliwa.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, mripuko mwingine wa homa ya manjano nchini Nigeria ulisababisha vifo vya watu tisa katika jimbo la Edo, kusini mwa nchi hiyo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya manjano vinatokea katika bara la Afrika.
Novemba mwaka jana, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kuwa watu 10 wamepoteza maisha kutokana na homa ya manjano kusini magharibi Ethiopia.
Aidha kati ya Disemba mwaka 2016 na tarehe 23 mwezi Aprili 2017, wanawake 25 wajawazito walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, huku kesi 135 zikiripotiwa katika kambi ya wakimbizi eneo la Diffa, kusini mwa Niger.