Mahakama yamuachia huru kinara wa upinzani Cameroon kufuatia agizo la rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56442-mahakama_yamuachia_huru_kinara_wa_upinzani_cameroon_kufuatia_agizo_la_rais
Mahakama ya Kijeshi ya Cameroon imemuachia huru kiongozi wa upinzani nchini humo Maurice Kamto, kufuatia agizo lililotolewa na Rais Paul Biya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2019 23:19 UTC
  • Mahakama yamuachia huru kinara wa upinzani Cameroon kufuatia agizo la rais

Mahakama ya Kijeshi ya Cameroon imemuachia huru kiongozi wa upinzani nchini humo Maurice Kamto, kufuatia agizo lililotolewa na Rais Paul Biya.

Rais Biya ametoa amri ya kufutwa mashitaka yote yaliyokuwa yakimkabili mwanasiasa huyo wa upinzani. Waziri Mkuu wa Cameroon Joseph Dion Ngute amesema kwa mujibu wa katiba, Rais wa Jamhuri, anayo haki ya kusimamisha kesi ikiwa anaona kuwa kusitishwa kwa kesi hiyo kuna faida kubwa kwa maslahi ya taifa.

Awali Rais Biya aliamuru pia kuachiliwa huru kwa wafungwa 333 wanaotuhumiwa kuhusika na mgogoro uliozuka katika maeneo yanayozungumza Kiingereza, wakati mazungumzo ya amani yalipokuwa yakiendelea.

Mazungumzo makubwa ya kusaka amani na kufikia mapatano ya kitaifa kati ya serikali ya Cameroon na wapinzani wa maeneo yanayozungumza Kiingereza yalimalizika Ijumaa ya tarehe 4 Oktoba mjini Yaounde.

Rais Paul Biya wa Cameroon

Hata hivyo kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha Renaissance Cameroon, Maurice Kamto na pia kutoshiriki mazungumzo hayo kiongozi mkuu wa Wacameroon wanaopigania kujitenga katika maeneo ya nchi hiyo yanayozungumza Kiingereza ni katika mambo yaliyoyafanya mazungumzo hayo yakose sura na uakilishi wa kitaifa.

Julius Ayuk Tabe, aliyejitangaza kuwa rais wa Ambazonia anatumikia kifungo cha maisha jela tangu miezi michache iliyopita katika gereza kuu la Yaoundé.