Walioteka nyara wanafunzi wa kike Nigeria wataka kikomboleo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56443-walioteka_nyara_wanafunzi_wa_kike_nigeria_wataka_kikomboleo
Watu wenye silaha waliowateka nyara wanafunzi sita wa kike wa chuo kimoja pamoja na wafanyakazi wawili wa chuo hicho huko Kaduna Nigeria, wametaka walipwe fedha za kuwakombolea mateka hao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 05, 2019 23:20 UTC
  • Walioteka nyara wanafunzi wa kike Nigeria wataka kikomboleo

Watu wenye silaha waliowateka nyara wanafunzi sita wa kike wa chuo kimoja pamoja na wafanyakazi wawili wa chuo hicho huko Kaduna Nigeria, wametaka walipwe fedha za kuwakombolea mateka hao.

Mkuu wa mkoa wa Kaduna wa kaskazini mwa Nigeria amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa watu hao wamesema kuwa wanataka walipwe fedha ndipo watawaachilia huru wanafunzi hao wa kike wa chuo cha Engravers na wasimamizi wao wawili.

Malam Nasir Ahmad el-Rufai amesema, hadi hivi sasa haijajulikana ni akina nani hasa waliwateka nyara wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho, na hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na utekaji nyara huo hadi hivi sasa. Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa mazungumzo yaliyofanyika hadi hivi sasa kupitia njia za siri, watekaji nyara hao wamesema tu wanataka walipwe fedha za kuwakomboa mateka hao bila ya hata kusema ni kiwango gani hasa cha fedha wanazotaka.

Utekaji nyara wanafunzi wa kike ni jambo lililoenea sana nchini Nigeria

 

Siku ya Alkhamisi jeshi la polisi la Nigeria lilitangaza habari ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana, wanafunzi sita wa Chuo cha Engravers pamoja na wafanyakazi wawili wa chuo hicho katika maeneo ya ndani kabisa ya kusini mwa jimbo la Kaduna.

Mwaka 2014 pia zaidi ya wanafunzi 270 wa kike walitekwa nyara na genge la kigaidi la Boko Haram mjini Chibok Nigeria. Wasichana 106 miongoni mwao walikombolewa, 60 walifanikiwa kutoroka na hadi hivi sasa hatima ya wanafunzi 100 kati ya hao haijulikani.