WHO: Kujiua ndiyo sababu kuu ya vifo vya watu nchini Uganda
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa karibu asilimia 10 ya vifo vya watu nchini Uganda vinatokana na kujiua.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani imesema na kuchapishwa leo katika gazeti la New Vision kuwa kila mwaka watu laki nane hufariki duniani kutokana na kujiua katika pembe mbalimbali za dunia na kwamba kiwango hicho nchini Uganda ni cha asilimia 10.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Magonjwa ya Akili nchini Uganda, Derrick Kizza amesema kujiua kunashika nafasi ya kwanza ya sababu za vifo nchini Uganda na kwamba idadi ya watu wanaojiua wenyewe nchini humo ni kubwa zaidi ya wale wanaoaga dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na virusi ya HIV.

Kizza anasema kwamba, idadi ya watu wanaoaga dunia kwa kujiua yumkini ikawa kubwa zaidi ya ile iyoripotiwa kwa sababu mara nyingi, kesi za kujiua huwa haziripotiwi kwa sababu watu huogopa kufanyiwa uchunguzi kama washukiwa.
Ni vyema pia kukumbusha kuwa, kujiua kunatajwa kuwa sababu ya pili ya vifo dunia kati ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 29, na asilimia 78 ya vijana hawa ni kutoka nchi zenye kipato cha chini na cha kati ikiwemo Uganda.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani inasema kuwa, kiwango cha kujiua watu dunia kimepungua kwa ujumla katika kipindi cha mwaka 2010 na 2016 kwa asilimia 9/8 lakini kimeongezeka katika bara la America.