Nov 07, 2019 01:13 UTC
  • Watu 37 wauawa katika shambulizi dhidi ya mgodi wa dhahabu Burkina Faso

Kwa akali watu 20 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, baada ya watu waliobeba silaha kushambulia mgodi wa dhahabu kaskazini mwa Burkina Faso.

Duru za habari zinaarifu kuwa, watu wasiojulikana ambao walikuwa wamejizatiti kwa silaha wamevamia mgodi unaomilikiwa na kampuni moja ya Canada katika kijiji cha Dolmane katika mkoa wa Soum kaskazini mwa nchi na kutekeleza ukatili huo.

Ingawaje hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini magenge yenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIS yamekuwa yakitekeleza ukatili wa aina hii nchini Burkina Faso na katika nchi jirani ya Mali.

Hii sio mara ya kwanza kwa magaidi kushambulia wafanyakazi wa migodi ya dhahabu nchini Burkina Faso. Mapema mwezi uliopita wa Oktoba, watu wasiojulikana walivamia mgodi mwingine wa dhahabu katika kijiji cha Madudaji katika mkoa wa Sam kaskazini mwa nchi na kuua makumi ya watu.

Magenge ya wabeba silaha yanayofanya mashambulizi Burkina Faso

Aidha mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wengine 16 waliuawa katika kile kinachosadikika kuwa ni shambulizi la kigaidi kaskazini mwa nchi. 

Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, magenge ya kigaidi yameongeza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali hasa ya kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Hadi hivi sasa watu wasiopungua 585 wameshauawa kwenye mashambulio hayo.

Tags