Waislamu Nigeria wakanusha madai ya polisi kumhusu Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57348-waislamu_nigeria_wakanusha_madai_ya_polisi_kumhusu_zakzaky
Wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamekanusha vikali madai ya Idara ya Kiitelejensia ya Nigeria kuwa polisi ya nchi hiyo inamzuilia mwanaharakati huyo wa Kiislamu kutokana na ombi na uamuzi wake mwenyewe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2019 08:18 UTC
  • Waislamu Nigeria wakanusha madai ya polisi kumhusu Zakzaky

Wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamekanusha vikali madai ya Idara ya Kiitelejensia ya Nigeria kuwa polisi ya nchi hiyo inamzuilia mwanaharakati huyo wa Kiislamu kutokana na ombi na uamuzi wake mwenyewe.

Katika taarifa, wafuasi hao wamesema idara hiyo ya kijasusi inaenda kinyume na sheria zilizoiunda, na kwamba madai yao kuhusu kuzuiliwa Sheikh Zakzaky hayana msingi wowote.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, "Haiwezekani Sheikh Zakzaky binafsi ameridhia kuendelea kuzuiliwa, angeulizwa angefadhilisha kuachiwa huru."

Idara ya Kiitelejensia ya Nigeria imetoa taarifa ikidai kuwa, Sheikh Zakzaky mwenyewe aliviomba vyombo vya mahakama viendelee kumzuilia katika jela yake ya siri, mara tu aliporejea kutoka India, alikoenda kwa ajili ya matibabu.

Sheikh Zakzaky na timu ya madaktari kutoka India

Baada ya jitihada kubwa, maandamano ya kila pembe na mashinikizo mengi ya ndani na kimataifa, mnamo mwezi Agosti mwaka huu, mahakama ya Nigeria ilimruhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wapelekwe India kutibiwa, lakini kutokana na matatizo na vizuizi vilivyowekwa na maafisa wa usalama walioandamana naye, kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe waliamua kurudi Nigeria baada ya kukaa India kwa muda wa siku mbili tu pasi na kupatiwa matibabu.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Disemba 2015 wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kushambulia Hussainiyah iliyoko katika mji wa Zaria, ambapo mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi.