Putin asisitiza ulazima wa kutatuliwa kwa amani mgogoro wa Libya
(last modified Fri, 27 Dec 2019 07:25:08 GMT )
Dec 27, 2019 07:25 UTC
  • Putin asisitiza ulazima wa kutatuliwa kwa amani mgogoro wa Libya

Rais wa Russia amemhutubu na kumsisitizia Waziri Mkuu wa Italia kuwa mgogoro wa Libya unapasa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani.

Rais Vladimir Putin aliyasema hayo jana katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte. Ikiashiria mazungumzo hayo ya simu ya Rais Putin na Waziri Mkuu wa Italia, Ofisi ya Rais wa Russia imeeleza kuwa viongozi wa nchi mbili hizo wanaunga mkono jitihada za kimataifa za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa.  

Putin ambaye kabla ya mazungumzo hayo alisema kuwa ni vigumu kuweka wazi ni nani mwenye haki huko Libya amesisitiza kuwa, Russia inawasiliana na Khalifa Haftar kamanda wa kundi la wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya na pia na Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo yenye makao yake magharibi mwa nchi inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya 

Libya sasa ina serikali mbili mashariki na magharibi mwa nchi tangu kupinduliwa dikteta wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.  

Jenerali mstaafu wa jeshi Khalifa Haftar anayedhibti upande wa mashariki mwa Libya anaungwa mkono na baadhi ya pande za kieneo na kimataifa zikiwemo Misri, Saudi Arabia, Imarati na Ufaransa. Mamia ya raia wameuawa na maelfu ya wengine wamekuwa wakimbizi tangu kujiri mashambulizi ya wanamgambo wanaoongozwa na jenerali huyo muasi kwa ajili ya kuudhibiti mji mkuu Tripoli kuanzia mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa.