Mapigano mapya yaua watu 14 magharibi mwa Niger
(last modified Sat, 28 Dec 2019 00:31:22 GMT )
Dec 28, 2019 00:31 UTC
  • Mapigano mapya yaua watu 14 magharibi mwa Niger

Watu wenye silaha wameshambulia msafara wa magari ya kijeshi katika eneo la Tillabéri la magharibi mwa Niger na kuua watu wasiopungua 14.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger imethibitisha habari hiyo katika taarifa yake ya jana Ijumaa na kuongeza kuwa, watu wenye silaha wametumia silaha nzito kushambulia msafara wa magari ya kijeshi uliokuwa unasindikiza maafisa wa uchaguzi katika kijiji cha Sanam na kupelekea watu wasiopungua 14 kuuawa.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger imeongeza kuwa, maafisa hao wa uchaguzi walikwenda kwenye eneo hilo ili kuandikisha wapiga kura kabla ya kushambuliwa na magenge ya watu wenye silaha.

Wanajeshi wa Niger katika operesheni ya kupambana na magenge yenye silaha

 

Wanajeshi wa Niger walilazimika kujibu mashambulizi ya watu hao na mapigano baina ya pande hizo mbili yaliendelea kwa muda. Taarifa hiyo inasema kuwa mwanajeshi mmoja wa serikali ya Niger hajulikani alipo inagawa hata hivyo watu hao wenye silaha walilazimika kukimbia baada ya kuzidiwa nguvu na kupata hasara kubwa.

Eneo la Tillabéri la magharibi mwa Niger liko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Mali. Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba hadi hivi sasa eneo hilo limekuwa kitovu cha mashambulizi makali ya watu wenye silaha. Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi 71 serikali ya Niger wameshauawa kwenye eneo hilo tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba.

Tags