ANC yailaani Marekani kwa kumuua Lt. Jen. Qassem Soleimani
(last modified Tue, 07 Jan 2020 04:28:03 GMT )
Jan 07, 2020 04:28 UTC
  • ANC yailaani Marekani kwa kumuua Lt. Jen. Qassem Soleimani

Chama tawala cha ANC cha Afrika Kusini kimetoa taarifa na kulaani hujuma ya Jeshi la Marekani ambayo ilipelekea kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC)

Katika taarifa ANC imesema: "Kitendo hicho kisicho cha ubinadamu ni hujuma dhidi ya mamlaka ya kujitawala na uhuru wa watu wa Iran. ANC inapinga vikali hujuma hii ya wazi dhidi ya watu na serikali ya Iran. Hujuma hii inaweza kulitimbukiza eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na dunia nzima katika vita." Taarifa hiyo imesema historia inaonyesha kuwa, waathirika wakubwa wa ugaidi kama huo wa Marekani ni wazee, watoto na wanawake huku vijana nao wakiathirika vibaya kutokana na kukumbwa na mustakbali mbaya. Taarifa hiyo ambayo imetiwa saini na katibu mkuu wa ANC Ace Magashule imesema: "ANC na harakati zote zinazopenda maendeleo duniani haziwezi kunyamaza kimya wakati kwa vitendo vyake, Marekani inavuruga amani na usalama duniani sambamba na kuvuruga kwa makusudi uthabiti wa kitaifa wa Iran." ANC imetoa wito kwa mataifa ya dunia, kupitia Umoja wa Mataifa kuchukua hatua imara kuzuia ugaidi wa kimataifa wa Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiswalisha Sala ya Maiti ya Shahidi Qassem Soleimani na mashahidi wenzake mjini Tehran 06-01-2020

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Ijumaa Alfajiri 3 Januari aliwasili nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo. Punde baada ya kuwasili, akiwa ndani ya gari pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashd al Shaabi pamoja na watu wengine wanane, walishambuliwa tokea angani na wanajeshi vamizi na wa kigaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na wote wakauawa shahidi katika tukio hilo.