Ripoti: Hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky yazidi kuwa mbaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58446-ripoti_hali_ya_kiafya_ya_sheikh_ibrahim_zakzaky_yazidi_kuwa_mbaya
Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetangaza kuwa, hali ya kiafya ya kiongozi huyo anayeshikiliwa gerezani imezidi kuwa mbaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2020 10:11 UTC
  • Ripoti: Hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky yazidi kuwa mbaya

Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetangaza kuwa, hali ya kiafya ya kiongozi huyo anayeshikiliwa gerezani imezidi kuwa mbaya.

Taarifa ya harakati hiyo iliyoandikwa katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter imeeleza kwamba, hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya sana.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema kuwa, taarifa ilizonazo kutoka kwa watu wa karibu waliofanikiwa kukutana na Sheikh Zakzaky zinaonyesha kwamba, hali ya kiafya ya mwanazuoni huyo imezidi kuwa mbaya kuliko hapo kabla.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu (Islamic Human Rights Commission (IHRC)) yenye makao yake London nchini Uingereza, Massoud Shajareh amezungumzia hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe na kusema: "Uwezekano wa kuachiwa huru mwanazuoni huyo ni mdogo sana hasa kwa kutilia maanani mashinikizo makubwa yanayofanywa na utawala wa Nigeria dhidi ya Sheikh Zakzaky."

Sheikh Ibrahim Zakzaky, (66) na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussaynia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.

Wanaharakati na wapigania haki katika maeneo mbalimbali ya dunia wameendelea kuitaka serikali ya Rais Muhamadu Buhari imuachilie huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.