Rais Nyusi wa Msumbiji aapishwa, upinzani wasusia
Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji alikula kiapo cha kulitumikia taifa jana Jumatano katika hafla iliyosusiwa na viongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo, wanaosisitiza kuwa kuliwepo na udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka uliomalizika wa 2019.
Akihutubia wananchi hususan wafuasi wa chama tawala katika sherehe hizo jijini Maputo, Rais Nyusi ameahidi kutumia muhula wake ujao wa miaka mitano kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika nchi hiyo. Amesema: "Amani imekuwa na itasalia kuwa kipaumbele chetu cha kwanza."
Wabunge na wafuasi wa vyama mashuhuri vya upinzani vya Momade na Renamo hawakuhudhuria hafla hizo ya kuapishwa Rais Nyusi.
Katibu Mkuu wa chama cha Renamo, Andre Magibire ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Sisi hatumtambui Nyusi kama kiongozi halali wa taifa, hata hivyo hatutajiingiza katika masuala ya ghasia na fujo ingawaje chama tawala kinatusukuma katika vita."

Msemaji wa chama tawala cha Frelimo, Caifadine Manasse amepuuzilia mbali madai hayo ya upinzani na kusisitiza kuwa, "Vyama vya upinzani vinatumia madai hayo ya uchakachuaji katika kura ili wasababishe ukosefu wa uthabiti nchini."
Novemba 2019, Mahakama ya Katiba Msumbiji ilitupilia mbali rufaa ya chama cha upinzani cha Renamo ambacho kilikuwa kinataka kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 15.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Rais Filipe Nyusi aliibuka mshindi wa kiti cha urais baada ya kujipatia asilimia 73 ya kura zote, huku Ossufo Momade kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Renamo akijipatia asilimia 21.88 ya kura.