WHO: Chanjo ya homa ya manjano ni sharti kwa waendao Angola
Shirika la Afya Duniani WHO limesema wasafiri wote wanaoenda nchini Angola wanahitaji kupata chanjo ya homa ya manjano ili kuthibitisha wamejikinga na kuzuia kuisambaza zaidi.
Tangazo hilo la WHO limekuja huku kukiendelezwa jitihada za kimataifa za kudhibiti kuenea kwa homa ya manjano nchini Angola.
Akizungumzia homa hiyo Jumanne, mkurugenzi mkuu wa WHO Daktari Margaret Chan amesema mlipuko huo wa Angola umejiri sambamba na kubainika pia kuenea ugonjwa huo katika nchi kadhaa za Afrika na Asia.
WHO imesema inahofia hasa maeneo ya mijini kuwa yako hatarini hivyo akasisitiza kila mtu ni lazima achanjwe kabla hajasarifi na abebe kadi ya kuthibitsha amepata chanjo hiyo.
Tarik Jašarević msemaji wa WHO anasema tangu kuzuka kwa ugonjwa huo Angola watu 258 wamepoteza maisha, visa zaidi ya 1,975 vinashukiwa na zaidi ya visa 600 vimethibitishwa maabarani.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya manjano vinatokea katika bara la Afrika.