Rwanda yasitisha mashtaka dhidi ya raia 17 wa Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59278-rwanda_yasitisha_mashtaka_dhidi_ya_raia_17_wa_uganda
Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imetangaza kuwa, nchi hiyo imesitisha mashtaka dhidi ya raia 17 wa Uganda waliokamatwa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2020 08:46 UTC
  • Rwanda yasitisha mashtaka dhidi ya raia 17 wa Uganda

Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imetangaza kuwa, nchi hiyo imesitisha mashtaka dhidi ya raia 17 wa Uganda waliokamatwa nchini humo.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya kuachiliwa huru raia 13 wa Rwanda waliokuwa wanashikiliwa nchini Uganda.

Taarifa hiyo imesema kupitia ubalozi wake mjini Kampala, serikali ya Rwanda imekaribisha kuachiwa huru kwa raia wake 13 na kurejeshwa Rwanda watuhumiwa wawili wa ugaidi waliohusika na shambulizi la Kinigi lililotokea Oktoba mwaka 2019.

Mapema mwezi huu, Rwanda na Uganda zilikubaliana kubalishana wafungwa ikiwa ni mojawapo ya njia za kuimarisha tena uhusiano kati ya nchi mbili hizo ambao umekuwa ukilegalega.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mkutano kati ya Marais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda uliofanyika katika mji mkuu wa Angola Luanda na kushuhudiwa pia na mwenyeji wao Joao Lourenco, na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mpaka wa Rwanda na Uganda

Itakuumbukwa kuwa, makubaliano ya kuondoa uhasama kati ya Rwanda na Uganda yaliyosainiwa na marais wa nchi hizo mbili, mwezi Agosti 2019, jijini Luanda nchini Angola yalileta ahueni na furaha kubwa kwa raia wa nchi hizo, hususan wafanyabiashara.

Uganda imekuwa ikiishtumu Rwanda kwa kutumia raia wake kuhatarisha usalama wake, huku Rwanda nayo ikiishtumu Uganda kwa kuwatesa na kuwazuia raia wake, suala ambalo lililisababisha Kigali kufunga mpaka wake wa Katuna.

Uhusiano kati ya Rwanda na Uganda uliharibika mwezi Februari mwaka jana wakati Rwanda ilipofunga mpaka wake mkuu, kwa madai kuwa Uganda inawahifadhi wahalifu wa Rwanda, madai ambayo yalijanushwa na serikali ya Uganda.

Joto la mzozo baina ya Rwanda na Uganda limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.