Mahakama Misri yawaondoa hatiani wanae Mubarak
Wana wawili wa kiume wa aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak wameondolewa hatiani na mahakama katika kesi iliyokuwa ikiwakabili ya uuzaji hisa za benki kinyume cha sheria miaka minne kabla ya mwamko wa mwaka 2011 uliopelekea baba yao kuondolewa madarakani baada ya miaka 30 ya utawala wake wa kidikteta.
Alaa na Gamal Mubarak pamoja na wengine saba walikuwa wanakabiliwa na mshtaka ya kupata faida kinyume cha sheria katika mchakato wa kuiuza Benki ya Al Watan ya Misri ambayo ilinunuliwa na Benki ya Kitaifa ya Kuwait mwaka 2007.
Wawili hao walisisitiza kuwa hawakuwa na hatia na walihuhduria kikao cha hukumu hiyo katika Mahakama ya Jinai ya Cairo. Wawili hao walitiwa mbaroni baada ya mwamko wa mwaka 2011 na walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela mwaka 2015, wakiwa pamoja na baba yao.
Ndugu hao wawili waliachiliwa huru punde baada ya hukumu hiyo kwa sababu tayari walikuwa wameshakaa muda mrefu kizuizini huku baba yao naye akiachiliwa huru mwaka 2017 baada ya kufutiwa mashtaka ya kuamuru waandamanaji wauawe.