Kutangaza utayari Khalifa Haftar wa kukubali usitishaji vita kwa masharti nchini Libya
Katika hali ambayo, vita nchini Libya vinaendelea na Waziri Mkuu wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Fayez al-Sarraj amesitisha ushiriki wake katika mazungumzo ya Geneva akilalamikia kuendelea mashambulio ya vikosi vya Khalifa Haftar, jenerali huyo muasi ametangaza utayari wake wa kuheshimu usitishaji vita lakini kwa masharti.
Jenerali Haftar, kiongozi wa vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya amesisitiza kuwa, kama kutakuweko na anga na mazingira maalumu yaani wanajeshi wa Uturuki na mamluki waondoke nchini Libya, basi yuko tayari kuheshimu usitishaji vita.
Licha ya juhudi zote za kieneo na kimataifa zenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya na kufanyika mikutano kadhaa katika miezi ya hivi karibuni kama mkutano wa Berlin ambapo kwa mujibu wake nchi waitifaki ziliahidi kuheshimu marufuku ya silaha dhidi ya Libya sambamba na kuandaa mazingira ya kupatikana usitishaji vita na kisha mazungumzo, lakini inaonekana juhudi hizo zote zimefeli na kutozaa matunda.
Mapigano nchini Libya yanaendelea katika hali ambayo, mivutano ya ndani hivi sasa imepelekea madola ajinabi na waingiliaji mambo wa kieneo kuingia rasmi katika nchi hiyo. Misri, Imarati, Jordan na Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi ambazo zimeingia katika uwanja wa vita Libya kwa maslahi ya Jenerali Khalifa Haftar na zimekuwa zikitoa misaada ya kifedha na kijeshi kwa vikosi vya jenerali huyo muasi.
Kushadidi mashambulio ya Haftar nchini Libya katika majuma ya hivi karibuni kwa himaya ya nchi tulizotaja, kumepelekea uharibifu mkubwa wa miundombinu ya nchi hiyo kama skuli, vituo vya elimu, hospitali na taasisi za mafuta na matokeo yake ni kupungua kwa usafirishaji nje mafuta ya nchi hiyo.
Mohammed al-Qablawi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya anasema: Uingiliaji wa Abu Dhabi na kumuunga mkono Khalifa Haftar na wanamgambo wake, ni hatua hasi na isiyokubalika. Hao wamekuwa chimbuko la uharibifu na mauaji ya raia wasio na hatia ndani ya Libya, na ni kwa sababu hiyo ndio maana watafuatiliwa na vyombo vya kimataifa vya mahakama.
Kushtadi mashambulio ya Khalifa Haftar kumeifanya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj iombe msaada kwa Uturuki kwa ajili ya kukabiliana na vikosi vya Haftar. Hivi sasa Uturuki imeingia katika vita vya Libya ikiiunga mkono serikali ya Fayyez al-Sarraj, hatua ambayo inalalamikiwa vikali na jenerali Haftar.
Jenerali huyo sambamba na kulaani hatua hiyo ya Uturuki amedai kwamba, vikosi anavyoviongoza vinapigana vikitekeleza jukumu lake la kuwalinda raia, mamlaka ya kujitawala nchi hiyo pamoja na mipaka ya nchi mkabala na uvamizi wa Uturuki.
Ahmed al-Mismar, msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya linaoongozwa na jenerali Haftar amesema kuwa, Uturuki imewaingiza nchini Libya kupitia viwanja vya ndege vya Misrata, Mitiga na Bandari ya Tripoli magaidi hatari kutoka Syria. Aidha anasema: Uturuki imetuma katika Bandari ya Tripoli manowari mbili za kivita, makombora na mfumo wa ulinzi wa makombora.
Filihali, Libya ni medani ya vita baina Haftar na waungaji mkono wake wa kigeni kwa upande mmoja na Fayez al-Sarraj na waungaji mkono wake kwa upande wa pili. Hii ni katika hali ambayo, mataifa yaliahidi kuheshimu marukufu ya silaha dhidi ya Libya na kujiepusha na utumaji silaha katika nchi hiyo. Inaonekana kuwa, vyanzo vya utajiri wa mafuta na gesi ya Mediterania, hamu ya kutaka jaha na ukubwa wa kieneo kupitia kuidhibiti Libya, ushindani wa kutaka madaraka na kubakisha satua katika mustakbali wa kisiasa wa eneo na vilevile uwezekano wa kupenya katika mataifa mengine ya Afrika kupitia nchini Libya ni mambo yenye msukumo mkubwa kwa madola yanayoingilia masuala ya ndani ya Libya.
Siku chache zilizopita, Fayez al-Sarraj, Mkuu wa Baraza la Uongozi na Waziri Mkuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa alisitisha ushiriki wake katika mazungumzo huko Geneva akilalamikia mashambulio ya mizinga ya Khalifa Haftar dhidi ya mji mkuu Tripoli. Hivi sasa Haftar sambamba na kulaani hatua hiyo ya Fayez al-Sarraj amesema kuwa, sharti lake la kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita ni kuondoka Uturuki katika ardhi ya Libya.
Utunishaji misuli huu wa kidiplomasiia sambamba na kuendelea vita na mapigano, kunazidi kutishia kugawanyika Libya na kutumwa vikosi vya kigeni katika nchi hiyo. Kwa mara nyingine tena macho na masikio ya walimwengu yameelekea katika meza ya mazungumzo ambayo mara hii yamepangwa kufanyika tarehe 26 ya mwezi huu wa Februari huko Geneva Uswisi.