Afrika Kusini kujenga uzio katika mpaka wake na Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59863-afrika_kusini_kujenga_uzio_katika_mpaka_wake_na_zimbabwe
Serikali ya Afrika Kusini imesema inajiandaa kujenga uzio wa kilomita 40 katika mpaka wa nchi hiyo na Zimbabwe, kwa lengo la kuzuia wahamiaji haramu kuingia nchini humo, na pia kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Corona nchini humo.
(last modified 2026-02-02T06:45:47+00:00 )
Mar 20, 2020 13:27 UTC
  • Afrika Kusini kujenga uzio katika mpaka wake na Zimbabwe

Serikali ya Afrika Kusini imesema inajiandaa kujenga uzio wa kilomita 40 katika mpaka wa nchi hiyo na Zimbabwe, kwa lengo la kuzuia wahamiaji haramu kuingia nchini humo, na pia kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Corona nchini humo.

Idara ya Miundomsingi nchini humo imesema ujenzi wa uzio huo utakaokuwa na urefu wa mita 1.8 utakamalika katika kipindi cha mwezi mmoja ujao. Hata hivyo idara hiyo haijaainisha kiwango cha fedha kitakachotumika katika mradi huo.

Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo ameagiza kufungwa kwa vituo 35 kati ya 53 vya mpaka wa nchi hiyo ya kusini wa Afrika, kama mojawapo ya hatua za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 nchini humo.

Waziri wa Ujenzi nchini humo, Patricia de Lille amesisitiza kuwa, ujenzi wa uzio huo mpakani na Zimbabwe si hatua ya kibaguzi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. 

Hivi karibuni Afrika Kusini ilishuhudia wimbi la hujuma dhidi ya wahajiri wa Kiafrika

Ameeleza bayana kuwa, "ujenzi huu wa ukuta ni kwa ajili ya kuwalida wananchi wa Afrika Kusini na watu wanaoingia hapa nchini."

Huku hayo yakiarifiwa, Wizara ya Afya ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, idadi ya watu walioambukizwa kirusi hatari cha Corona nchini humo hadi sasa imeongezeka na kufikia watu 202.

Kesi za maambukizi ya virusi vya COVID-19 barani Afrika zimepindukia 800 hadi kufikia sasa.