Apr 07, 2020 07:37 UTC
  • Makumi ya askari wauawa katika shambulizi la kigaidi nchini Mali

Makumi ya wanajeshi wa Mali wameuawa katika shambulio la magaidi dhidi ya kambi moja ya jeshi katika eneo la Bamba jimboni Gao, kaskazini mwa nchi.

Serikali ya Mali imetoa taarifa ikisema kuwa, askari 25 wameuawa na wengine 6 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Aidha wanamgambo zaidi ya kumi wametimuliwa na vikosi vya usalama vilivyofika kwenye eneo la tukio hilo ili kulisaidia jeshi la Mali.

Serikali ya Mali imelaani vikali shambulizi hilo ambalo ni katika wimbi la mashambulizi ya kigaidi linaloshuhudiwa nchini humo wakati huu ambapo dunia imezongwa na janga la corona.

Mwezi uliopita wa Machi, wanamgambo waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya jeshi huko kaskazini mashariki mwa nchi ya Mali na kuua wanajeshi wasiopungua 30 wa serikali ya nchi hiyo.

Wanajeshi wa Mali wakilinda doria

Katika miaka ya hivi karibuni nchi ya Mali imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya waasi na magaidi wa makundi ya al Qaida na Daesh (ISIS). 

Mwaka 2013 Umoja wa Mataifa ulituma kikosi cha askari wa kimataifa cha MINUSMA  nchini Mali kwa ajili ya kukabiliana na waasi na wanamgambo hao kikishirikiana na wanajeshi wa Ufaransa. Hata hivyo askari hao wa UN na wa Ufaransa hawajafanikiwa kurejesha amani na utulivu  nchini Mali na nchi hiyo bado inakabiliwa na tishio kubwa la makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji ya mara kwa mara.  

Tags