WHO yatangaza mlipuko wa homa ya njano Sudan Kusini
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza habari ya mlipuko wa homa ya njano katika maeneo ya kusini mwa Sudan Kusini.
Katika taarifa, taasisi hiyo ya afya ya Umoja wa Mataifa imesema kesi mbili za homa ya njano zimetambuliwa katika eneo la Kajo-keji, mpakani mwa Sudan Kusini na Uganda.
Wizara ya Afya ya Sudan Kusini kwa kushirikiana na WHO inatazamiwa kuzindua chanjo ya homa ya njano katika eneo lililoathiriwa, huku chanjo ya kinga ya homa hiyo hatari ikitazamiwa kuzinduliwa kufikia mwaka 2022.
Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika imeripoti milipuko kadhaa ya homa ya njano katika miaka ya huko nyuma. Mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa huo ni ule wa Mei mwaka 2003 katika jimbo la Imatong, ambapo watu 27 waliaga dunia, huku jumla ya kesi 178 zikiripotiwa.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya njano vinatokea katika bara la Afrika.
Disemba mwaka 2018, mripuko wa homa ya njano nchini Nigeria ulisababisha vifo vya watu tisa katika jimbo la Edo kusini mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.