Magaidi 126 na askari 15 wauawa katika mapigano makali Misri
Jeshi la Misri limesema askari wake 15 wameuawa katika mapigano makali na magaidi ambapo magaidi 126 wakufurishaji pia wameuawa mashariki mwa nchi.
Katika taarifa ya Jumapili, Jeshi la Misri limesema kufuatia oparesheni ya kuangamiza makundi ya magaidi na wabeba silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini mwa nchi hiyo, maafisa 7 na askari 8 wameuawa. Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, katika oparesheni 16 kaskazini na kati mwa mkoa huo katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, magaidi wakufurishaji wapatao 126 wameuawa na idadi kubwa ya silaha zao zimenaswa.
Taarifa hiyo imesema magaidi 266 wamekamatwa katika oparesheni hizo.
Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri jana Jumapili ilitangaza kuwa, magaidi wengine 18 wameuawa katika mapigano na wanajeshi kando kando ya mji wa Bir al-Abed mkoani Sinai Kaskazini. Mapigano hayo yalijiri baada ya magaidi kutega bomu ambalo iliwalenga maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda doria.
Tokea mwaka 2018, Jeshi la Misri limekuwa likitekeleza oparesheni maalumu dhidi ya makundi ya kigaidi katika eneo la Sinai mashariki mwa nchi hiyo.
Wakuu wa Misri wanasema tokea wakati huo, magaidi 650 wameuawa huku askari 50 nao wakipoteza maisha katika oparesheni hizo za usalama.
Makundi ya kigaidi huko Misri yameshadidisha hujuma na mashambulizi yake katika mkoa wa Sinai ya Kaskazini na wakati huo huo pia yanafanya hujuma katika maeneo ya katikati na kusini mwa Sinai au katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Kundi la magaidi wakufurishaji linaloitwa Ansarul Baitul Maqdis ambalo limebadili jina lake na kuwa kundi la Wilayat Sinai baada ya kuungana na kundi la kigaidi la Daesh ndilo linalotekeleza mashambulizi mengi dhidi ya wanajeshi wa Misri.
Idara za usalama za Misri zimetahadharisha kuwa upo uwezekano kundi la Daesh likatumia vibaya hali ya sasa ya maambukizi ya corona duniani kushadidisha mashambulizi yake.