Ethiopia yaituhumu Misri kuwa imechochea ghasia na machafuko nchini humo
(last modified Thu, 04 Jun 2020 11:43:55 GMT )
Jun 04, 2020 11:43 UTC
  • Ethiopia yaituhumu Misri kuwa imechochea ghasia na machafuko nchini humo

Afisa wa serikali ya jimbo la Oromia nchini Ethiopia ameituhumu serikali ya Misri kuwa imechochea maandamano na ghasia zilizoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni jimboni humo.

Addisu Arega amesema kuwa serikali ya jimbo la Oromia ambalo ndilo kubwa zaidi nchini Ethiopia, ina ushahidi unaothibitisha kwamba, serikali ya Misri imehusika katika kuchochea machafuko ya wapinzani wa serikali kutokana na hitilafu za Addis Ababa na Cairo kuhusu kadhia ya ujenzi wa bwawa la al Nahdha juu ya maji ya Mto Nile.

Amesema Ethiopia haitalegeza kamba hata kidogo katika masuala yanayohusiana na usalama wake na kwamba iwapo kutatokea lolote wahusika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.   

Addisu Arega ambaye ni makamu wa rais wa jimbo la Oromia amesema kuwa Ethiopia ina haki ya kutumia maliasili zake na kwamba Misri inafanya jitihada za kuinyima haki hiyo kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchochea wapinzani wa serikali kufanya fujo na ghasia katika jimbo hilo. Amesema serikali ina ushahidi unaothibitisha kuwa, serikali ya Misri inahusika katika machafuko yaliyotokea karibuni na kusababisha uharibifu na ukosefu wa amani.

Kiongozi huyo amewataka Waethiopia kuwa macho na wasikubali kutumiwa kama wenzo wa kutimiza malengo ya nchi za kigeni.

Ethiopia inahitilafiana na nchi za Misri na Sudan kuhusu ya suala la ujenzi wa bwawa la al Nahdha juu ya maji ya Mto Nile.

Tags