Waziri wa zamani wa Misri: Israel ni adui wa kiistratajia wa Wamisri
(last modified Mon, 08 Jun 2020 02:38:14 GMT )
Jun 08, 2020 02:38 UTC
  • Waziri wa zamani wa Misri: Israel ni adui wa kiistratajia wa Wamisri

Waziri wa zamani wa Misri ameutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kama adui wa kistratajia wa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Tovuti ya habari ya Okaz imemnukuu Mohammed Nasruddin, aliyekuwa Waziri wa Unyunyizaji wa Misri akisema hayo na kuongeza kuwa, "Tel Aviv inafanya jitihada nyuma ya pazia za kuwaweka wananchi wa Misri katika matatizo na hali ngumu."

Kadhalika ameutuhumu utawala huo haramu kuwa unafanya hila ya kuficha mgogoro wa Bwawa la al-Nahdha, mbali na kuiunga mkono Ethiopia na kuwawekea vizuizi wananchi wa Misri wasiweze kustafidi na Mto Nile.

Kwa mujibu wa waziri huyo wa zamani wa unyunyizaji wa Misri, nchi hiyo ya Kiarabu inapaswa kushirikiana na Ethiopia na Sudan katika kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Bwawa la al-Nahdha.

Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri amekuwa akikosolewa kwa kuwa na uhusiano na Israel

Jitihada za Marekani za kujaribu kutatua mgogoro juu ya bwawa hilo ziligonga mwamba miezi michache iliyopita. Tarehe 29 Februari, kulifanyika mkutano mjini Washington ambao ulisusiwa na Ethiopia na ndani ya mkutano huo kulitiwa saini makubaliano ya mpango wa Marekani kuhusu bwawa hilo.

Ethiopia ilitangaza kupinga mpango huo na ikaishambulia taarifa iliyotolewa na Marekani ya kutaka kuanza tena mazungumzo kuhusu ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha unaotajwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa umeme barani Afrika. 

Tags