Jun 12, 2020 02:33 UTC
  • Shambulizi la kigaidi laua wanajeshi 10 wa Ivory Coast

Kwa akali askari 10 wa Jeshi la Ivory Coast wameuawa katika shambulizi la genge moja la wanamgambo katika mpaka wa nchi hiyo na Burkina Faso.

Hili ni shambulio la kwanza la kigaidi katika ardhi ya Ivory Coast tokea Machi mwaka 2016, baada ya magaidi kushambulia mgahawa wa kifahari wa Grand Bassam ambapo watu 19 waliuawa. Shambulizi hilo lilifanywa na wanachama wa mtandao wa al-Qaeda katika eneo la Sahel kaskazini mwa Afrika.

Katika hujuma ya alfajiri ya jana Alkhamisi, magaidi hao walivamia kwa risasi kituo cha kiusalama katika eneo la Kafolo kaskazini mwa nchi na kuua wanajeshi wasiopungua 10.

Lassina Doumbia, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Ivory Coast amethibitisha habari hiyo ya kuuawa wanajeshi 10 wa nchi hiyo, mbali na wengine saba kujeruhiwa.

Askari wa Ivory Coast wakishika doria

Baadhi ya duru za habari zinasema idadi ya wanajeshi waliouawa katika hujuma hiyo ni 11 pamoja na afisa mmoja wa polisi; na kwamba gaidi mmoja ameangamizwa pia katika shambulio hilo. 

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, huenda waliotekeleza shambulizi hilo la jana ni wanachama wa genge la kigaidi waliojipenyeza nchini humo wakitokea nchi jirani ya Burkina Faso.

Tags