Jun 15, 2020 03:10 UTC
  • Wanajeshi 2 wa kulinda amani wa UN wauawa nchini Mali

Askari wawili wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani nchini Mali (MINUSMA) wameuawa katika shambulizi lililotokea kaskazini mwa nchi hiyo.

Hayo yalisemwa jana Jumapili na Mahamat Saleh Annadif, mkuu wa kikosi hicho cha UN nchini Mali na kuongeza kuwa, wanajeshi hao waliuawa katika shambulizi la juzi Jumamosi.

Amesema askari hao wa MINUSMA waliuawa baada ya msafara wa kilojistiki wa kikosi hicho kushambuliwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wamejizatiti kwa silaha, katika barabara kuu iliyoko baina ya miji ya Tessalit na Gao, kaskazini mwa nchi.

Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo inayoaminika kuwa ya kigaidi.

Hii ni katika hali ambayo, wiki iliyopita raia wasiopungua 43 waliuawa katika mashambulio mawili yaliyofanywa na watu wenye silaha nchini Mali. 

Askari wa MINUSMA nchini Mali

Baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo yanadhibitiwa na magenge ya kigaidi yenye mfungano na Daesh (ISIS) na mtandao wa al-Qaida ambayo yanafanya mashambulizi ya kutisha na ya kikatili katika miaka ya hivi karibuni, si nchini Mali tu, bali hadi katika nchi zinazopakana na nchi hiyo.

Hii ni licha ya uwepo wa kikosi cha askari wa Kofia Buluu wa UN kwa jina la MINUSMA nchini Mali tokea mwaka 2013.

Tags