Vigogo wa upinzani Uganda waunda muungano kukabiliana na Museveni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61620-vigogo_wa_upinzani_uganda_waunda_muungano_kukabiliana_na_museveni
Viongozi wa upinzani nchini Uganda wametangaza kuunda muungano mpya kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Yoweri Museveni ambaye ameitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 34 sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2020 10:46 UTC
  • Vigogo wa upinzani Uganda waunda muungano kukabiliana na Museveni

Viongozi wa upinzani nchini Uganda wametangaza kuunda muungano mpya kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Yoweri Museveni ambaye ameitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 34 sasa.

Kati ya waliounda muungano huo  ni kiongozi mkongwe wa upinzani Kizza Besigye wa chama cha FDC, ambaye amewahi kugombea urais mara kadhaa,   na mwanasiasa chipukizi Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Wengine walio katika muungano huo wa upinzani ni Meya wa Kampala Erias Lukwago wa chama cha DP, Rais wa chama cha CP Keny Lukyamuzi na rais wa chama cha JEEMA Asuman Basalirwa. Vinara hao wa upinzani wamezindua muungano huo kwa lengo la kuwa mgombe mmoja katika uchaguzi ujao mwaka 2021 dhidi ya Rais Museveni.

Besigye amekutana mara kadhaa na Bobi Wine kwa lengo la kuunda kile ambacho wanakitaja ni muungano wa pamoja na kuleta mabadiliko nchini humo.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Wanasiasa hao wameuunda muungano huo wao Jumatatu asubuhi walipokutana katika Wilaya ya  Wakiso nje kidogo ya mji mkuu, Kampala.

Chama tawala Uganda, NRM, tayari kimeshamtangaza Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 75, kuwa mgombea rasmi wa chama hicho katika uchaguzi wa rais mwakani. Museveni aliingia madarakani mwaka 1986 wakati alipochukua hatamu za uongozi baada ya vita vya miaka mitano na sasa yeye ni kati ya viongozi waliohudumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.