Wanajeshi watano wa Misri wauawa katika mkoa wa Sinai
Duru za kijeshi za Misri zimetangaza habari ya kuuawa wanajeshi watano wa nchi hiyo katika shambulio lilifanywa na watu wenye silaha katika eneo la Sinai la kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Jana usiku televisheni ya al Jazeera ya Qatar ilizinukuu duru za kijeshi za Misri zikisema kwamba watu wenye silaha wamewashambulia wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo la Sinai na kuua wanajeshi watano.
Polisi na wanajeshi wa Misri wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na watu wenye silaha ambao wana maficho yao mengi kaskazini mwa Misri.
Ngome za magenge hayo ziko katika mkoa wa Sinai Kaskazini ambapo kundi hatari zaidi kuliko yote ni lile linalojiita Answar Bayt al Muqaddas ambalo limetangaza rasmi utiifu wake wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na limebadilisha jina na kujiita Wilayat Sinai.
Mwezi uliopita wa Mei, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilisema kuwa, wanachama 21 wa genge moja la kigaidi wamuawa katika operesheni mbili tofauti zilizofanywa na jeshi la Misri katika Peninsula ya Sinai. Wizara hiyo ilisema pia kuwa, maafisa wawili wa serikali ya Misri wamejeruhiwa kwenye operesheni hizo dhidi ya maficho ya magaidi.
Mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mapigano baina ya maafisa usalama na magenge ya kigaidi ambayo yameshadidisha mashambulizi yake katika miaka ya hivi karibuni, hususan baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mohammad Morsi hapo mwaka 2013.