Kuongezeka jitihada za kutatua mgogoro wa bwawa la al Nahdha
Hitilafu zinazoendelea baina ya nchi za Misri, Sudan na Ethiopia kuhusu ujenzi wa bwawa na al Nahdha juu ya maji ya Mto Nile na mgogoro uliosababishwa na hitilafu hizo zimezidisha jitihada za kikanda na kimataifa za kutafuta suhulisho la hitilafu hizo.
Katika uwanja huo, imepangwa kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya kikao Jumatatu ijayo kujadili maudhi ya bwawa la al Nahdha. Kabla ya kufanyika kikao hicho, viongozi wa nchi za Misri, Sudan na Ethiopia wamekutana na wajumbe wa kamati kuu ya Umoja wa Afrika na kuafikiana kujiepusha na hatua yoyote ya upande mmoja ikiwa ni pamoja kujaza maji katika bwawa la al Nahdha kabla ya kufikiwa mapatano.
Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok amesema: Katika kikao cha Umoja wa Afrika tumekubaliana kwamba kuna udharura wa kufikiwa maafikiano yatakayokidhi maslahi ya nchi tatu kuhusu bwawa la al Nahdha, na imeamuliwa kwamba, nchi tatu zijiepushe kuchukua hatua yoyote ya upande mmoja ikiwa ni pamoja na kujaza maji katika bwawa hilo kabla ya kufikia mapatano.
Ujenzi wa bwawa la al Nahdha unaofanyika nchini Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile umezusha mgogoro mkubwa baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan. Vikao mbalimbali vya usuluhishi vinavyofanyika tangu mwaka 2011 havijaweza kupata ufumbuzi wa mgogoro huo. Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba, ujenzi wa bwawa la al Nahdha na kuanza kufanya kazi bwawa hilo kutapunguza mgao wa maji wa nchi hizo. Misri inatambua ujenzi wa bwawa hilo kuwa ni tishio kwa usalama wake wa kitaifa kwa sababu karibu asilimia 90 ya mahitaji yake ya maji yanadhaminiwa kutokana na Mto Nile. Kwa sababu hiyo kadhia ya bwawa la al Nahdha limezusha mgogoro mkubwa baina ya Cairo na Addis Ababa katika miezi ya hivi karibuni kiasi kwamba, Misri imetishia kutumia nguvu za jeshi kwa ajili ya kuzuia ujenzi huo. Hata hvyo Ethiopia inasisitiza kuwa, bwawa hilo litaanza kufanya kazi mwezi Julai mwaka 2020 kama ilivyopangwa, hata kama hakutafikiwa mapatano baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan. Msimamo huu umezidisha wasiwasi wa nchi za Misri na Sudan.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan, Asma Mohamed Abdalla amesema: Khartoum inapinga vikali hatua yoyote ya kuanza kazi bwawa la al Nahdha kabla ya kufikiwa makubaliano yanayokidhi maslahi ya nchi zote husika. Pande zote zinapaswa kujiunga na mwenendo wa mazungumzo kwa nia njena na kwa kuzingatia sheria za kimataifa ili kuweza kudhamini maslahi ya mataifa ya Sudan, Misri na Ethiopia."
Baada na kushindwa mazungumzo ya awali baina ya nchi hizo tatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri pia ilitoa taarifa ikitangaza kuwa: Kwa kutegemea kifungu cha 35 cha hati ya Umoja wa Mataifa kinachoziruhusu nchi wanachama kuripoti mgogoro wa aina yoyote unaohatarisha amani na usalama wa kimataifa katika Baraza la Usalama, Cairo imechukua uamuzi wa kulitaka baraza hilo kuingilia mgogoro wa bwawa la al Nahdha.
Jumatatu wiki hii Baraza la Usalama linatarajiwa kuitisha kikao cha kujadili stratijia ya kutatua mgogoro huo baada ya nchi tatu Misri, Ethiopia na Sudan kukubaliana kwamba hazitachukua hatua yoyote ya upande mmoja kabla ya kufikia mapatano. Msimamo huu unazidisha matumaini ya kupatikana mwafaka na suluhisho la mgogoro huo. Hata hivyo suala linalotia wasiwasi mkubwa ni uingiliaji wa nchi na tawala za kigeni katika kadhia hiyo.
Ujenzi wa bwawa la al Nahdha na suala la mgao wa maji ya Mto Nile, matukio ya kisiasa katika nchi za eneo hilo, hali inayotawala, harakati za tawala za kibeberu hususan utawala wa Kizayuni wa Israel na misaada yake kwa Ethiopia katika ujenzi wa bwawa hilo, na vilevile hitilafu zinazozushwa na Tel Aviv baina ya Ethiopia na nchi mbili za Misri na Sudan kwa ajili ya kudhamini maslahi yake haramu, yote hayo yamesababisha hali tete na mgogoro mkubwa. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, kuna udharura wa kupatikana ufumbuzi wa kadhia hiyo juu ya jinsi ya kugawana kwa uadilifu maji ya Mto Nile kwa shabaha ya kudumisha amani na usalama katika eneo hilo la Afrika.