Ethiopia: Marekani ikome kuiunga mkono Misri kibubusa
(last modified Mon, 29 Jun 2020 03:56:39 GMT )
Jun 29, 2020 03:56 UTC
  • Ethiopia: Marekani ikome kuiunga mkono Misri kibubusa

Gazeti moja la Ethiopia limeishambulia vikali serikali ya Marekani kwa kile lilichosema ni uungaji mkono wa kibubusa na kipofupofu wa misimamo ya Misri katika mazungumzo ya kutafuta suluhisho la bwawa na al Nahdha linalojengwa na Addis Ababa juu ya maji ya Nto Nile.

Gazeti la The Reporter limesema katika tahariri yake kwamba serikali ya Washington inapaswa kukomesha uungaji mkono wake kipofu na wa kibubusa kwa Misri katika mazungumzo ya bwawa la al Nahdha na inapaswa kutenda kama msimamizi asiyependelea upande wowote. Gazeti hilo limeongeza kuwa, Marekani haiwezi kuwa mpatanishi asiyependelea upande mmoja iwapo itaendelea kukariri misimamo isiyokubalika ya Misri.

The Reporter limeandika kuwa, taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani na ile iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu ambazo zote mbili ziliitahadharisha Ethiopia kujaza maji katika bwawa la al Nahdha kabla ya kufikiwa mapatano ya mwisho na Misri na Sudan, hazikubaliki.

Gazeti hilo limeongeza kuwa, Waethiopia hawaweza kusalimu amri mbele ya matakwa yanayowalazimisha kulegeza kamba mkabala wa mradi wa kitaifa wanaouthamini na kuupa umuhimu mkubwa.

Ujenzi wa bwawa la al Nahdha

The Riporter limeandika kuwa, jitihada za Marekani za kujaribu kuibana Ethiopia na kuiunga mkono nchi ambayo haichangii hata tole moja la maji katika Mto Nile ni kuidhalilisha Addis Ababa.

Ujenzi wa bwawa la al Nahdha unaofanyika nchini Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile umezusha mgogoro mkubwa baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan. Vikao mbalimbali vya usuluhishi vinavyofanyika tangu mwaka 2011 havijaweza kupata ufumbuzi wa mgogoro huo. Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba, ujenzi wa bwawa la al Nahdha na kuanza kufanya kazi bwawa hilo kutapunguza mgao wa maji wa nchi hizo. Misri inatambua ujenzi wa bwawa hilo kuwa ni tishio kwa usalama wake wa kitaifa kwa sababu karibu asilimia 90 ya mahitaji yake ya maji yanadhaminiwa kutokana na Mto Nile. 

Tags