Mgogoro wa Bwawa la Renaissance waingia Baraza la Usalama, Ethiopia yatahadharisha
Mgogoro wa Bwawa la Renaissance (Al Nahdha) baina ya Misri, Sudan na Ethiopia umewekwa rasmi kwenye meza ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Misri kuwasilisha muswada huo kwa ajili ya kujadiliwa na wanachama wa baraza hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry amesema nchi yake imewasilisha faili la mgogoro wa Bwawa la Renaissance kwenye meza ya Baraza la Usalama kwa ajili ya kujadiliwa na kwamba hatua hiyo inaafikiana na matokeo ya kikao cha ofisi ya Umoja wa Afrika kuhusiana na kadhia hiyo.
Shoukry amesema katika kikako cha Baraza la Usalama kilichofanyika kwa njia ya video kwamba, baraza hilo linapaswa kuipa kadhia hiyo umuhimu mkubwa ili kuepusha ghasia na machafuko zaidi katika eneo hilo la Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesisitiza kuwa ni kweli kwamba Bwawa la Renaissance lina umuhimu sana kwa ajili ya ustawi wa Ethiopia na watu wa nchi hiyo lakini kujazwa maji bwawa hilo bila ya muwafaka wa pande husika yumkini kukahatarisha maisha ya mamilioni ya Wamisri na Wasudani.
Kwa upande wake Ethiopia imetahadharisha kuwa hatua hiyo ya Misri ya kuliwasilisha rasmi faili la Bwawa la Renaissance katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yumkini ikatatiza mchakato wa kupata ufumbuzi wa kadhia hiyo.
Taye Atske Selassie Made amesema njia bora ya kutatua mgogoro huo ni kupeleka kadhia hiyo kwenye Umoja wa Afrika na kuzihamasisha nchi tatu husika, yaani Ethiopia, Sudan na Misri, kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Selassie Made amelitaka Baraza la Usalama la UN kuacha kukuza kupita kiasi hitilafu zilizopo baina ya Ethiopia na Misri, suala ambalo amesisitiza kuwa, yumkini likaharibu mafanikio yaliyopatikana hadi hivi sasa.
Ujenzi wa Bwawa la Renaissance unaofanyika nchini Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile umezusha mgogoro mkubwa baina ya nchi hiyo na nchi za Misri na Sudan.
Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba, ujenzi wa Bwawa la Renaissance na kuanza kufanya kazi bwawa hilo kutapunguza mgao wa maji wa nchi hizo. Misri inatambua ujenzi wa bwawa hilo kuwa ni tishio kwa usalama wake wa kitaifa kwa sababu karibu asilimia 90 ya mahitaji yake ya maji yanadhaminiwa kutokana na Mto Nile. Ethiopia inakanusha madai hayo ikisema Bwawa la Renaissance ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya taifa hilo.