Jul 02, 2020 06:38 UTC
  • Ugiriki yapinga hatua ya Uturuki ya kutuma jeshi nchini Libya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki amezitaja hatua za kijeshi za Uturuki huko Libya kuwa ni uvamizi na kusisitiza kuwa Athens inapinga hatua hizo.

Nikos Dendias kwa mara nyingine tena amelaani kuwepo majeshi ya Uturuki huko Libya na kutoa wito wa kusitishwa oparesheni za kijeshi za Ankara nchini humo. 

Dendias jana Jumatano alikutana na kufanya mazungumzo na Aguila Saleh, Spika wa Bunge la mashariki mwa Libya katika mji wa Qabe. Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki amesisitiza umuhimu wa kutafutwa njia ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki amewataka wanajeshi wote wa kigeni walioko Libya wakiwemo wa Uturuki kuondoka haraka nchini humo. 

Itafahamika kuwa, serikali ya Uturuki inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj. 

Fayez al Sarraj, Waziri Mku wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya 

Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa. Serikali ya mashariki mwa Libya inayoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar haitambuliki kimataifa. 

Tags