Rwanda yapiga marufuku mashirika, asasi kushirikiana na Ubelgiji
Serikali ya Rwanda imeyapiga marufuku mashirika yote ya kimataifa na ya kitaifa yasiyo ya kiserikali (NGOs) na mashirika yanayofanya kazi nchini humo kushirikiana na serikali ya Ubelgiji na mashirika yake tanzu.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Utawala ya Rwanda jana Alkhamisi imesema, "Kuanza kutekelezwa mara moja, ushirikiano wote, ubia, na miamala na serikali ya Ubelgiji na taasisi zake shirikishi, watendaji wa ushirikiano usio wa kiserikali, mashirika na wakala ni marufuku."
Imeeleza kuwa, “Miradi au mikataba yoyote inayoendelea inayohusisha taasisi hizi na taasisi nyingine zinazofanana lazima ikomeshwe mara moja na kuripotiwa ipasavyo.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hakuna ufadhili wowote, ikiwa ni pamoja na misaada na michango, itakayopokelewa au kutolewa kwa serikali ya Ubelgiji, taasisi zake, mashirika au wakala wake shirikishi.
Serikali ya Rwanda imesema kizuizi hicho kinajumuisha usaidizi wa bajeti, ufadhili wa mradi, ruzuku ya usaidizi wa kiufundi na malipo yanayofanywa kupitia wasuluhishi na wahusika wengine. Taarifa hiyo ya Bodi ya Utawala ya Rwanda imeonya kuwa, kutotekelezwa vikwazo hivyo kutasababisha kufutiwa usajili au hatua nyingine za kiutawala.
Hatua hiyo imekuja huku uhusiano baina ya nchi hizo mbili ukizidi kuharibika kutokana na mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Chini ya wiki mbili zilizopita, Ubelgiji ilijibu hatua ya Rwanda ya kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi hiyo ya Ulaya na kusema kuwa, wanadiplomasia wa Rwanda wanapaswa kuondoka nchini Ubelgiji.