May 02, 2016 03:59 UTC
  • Kikao cha Arusha kwa ajili ya amani ya Burundi chaahirishwa

Mazungumzo ya amani ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ambayo yalitazamiwa kuanza leo Jumatatu mjini Arusha nchini Tanzania yameahirishwa.

Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na duru za kidiplomasia zimedokeza kuwa mazungumzo hayo ambayo yalitazamiwa kuanza leo kwa kuzileta pamoja pande zote husika sasa yatafanyika tarehe 21 mwezi huu wa Mei.

Shirika la habari la AFP limewanukuu viongozi wa upinzani nchini Burundi wakithibitisha kuwa mazungumzo hayo hayatang'oa nanga leo kama ilivyotarajiwa. Mwanadiplomasia mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia AFP kuwa, ni vyema mazungumzo hayo yameahirishwa kwa kuwa baadhi ya wadau walisema wasingehudhuria kwa kuwa hawakupata mwaliko.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Bujumbura imesema haitahudhuria mazungumzo hayo eti kwa sababu haijapewa mwaliko rasmi.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 400 wameuawa na wengine karibu laki mbili na 60 elfu wamekuwa wakimbizi tangu mwezi Aprili mwaka jana, wakati Burundi ilipotumbukia kwenye machafuko yaliyotokana na Rais Nkurunziza kuamua kugombea tena urais kwa muhula wa tatu. Hata hivyo watetezi wa haki za binadamu nchini humo hivi karibuni waliuambia Umoja wa Mataifa kuwa idadi ya watu waliouawa kutokana na machafuko hayo yumkini imepindukia watu 1000.

Tags