Jul 17, 2020 08:00 UTC
  • Wanavijiji 12 wauawa Mali, huku mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa yakiendelea

Raia wasiopungua 12 wameuliwa baada ya watu wasiojulikana waliobeba silaha wakiwa wamepanda pikipiki kushambulia vijiji kadhaa vya wakulima wa kabila la Dogon katika eneo la Mopti, katikati mwa Mali.

Ali Dolo, meya wa mji ulio karibu na eneo la tukio amethibitisha habari hizo jana Alkhamisi na kuongeza kuwa, miongoni mwa waliouawa katika shambulizi hilo ni wakulima kumi waliokuwa mashambani wakiendelea na shughuli zao za kila siku.

Amesema lengo la mashambulizi hayo ni kuzuia shughuli za ukulima katika eneo hilo. Baadhi ya duru za habari zinaarifu kuwa, waliouawa katika shambulizi hilo la watu waliojizatiti kwa silaha ni watu 13.

Mapema mwezi huu pia, watu wasiopungua 32 waliuliwa katika hujuma nyingine ya watu wasiojulikana waliobeba silaha katika eneo hilo la Mopti, katikati mwa Mali. Mashambulio ya namna hii hufanywa na makundi yenye mielekeo ya kidini ambayo hudai yanawatetea wafugaji wa kabila la Fulani dhidi ya mahasimu wao wa kabila la Dogon ambao ni wakulima.

Maandamano ya ghasia yamemlazimisha Rais Keita kuvunja Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo

Haya yanajiri katika hali ambayo, rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan yuko mjini Bamako, akiongoza timu ya mazungumzo ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili Mali kwa wiki kadhaa sasa.

Watu wasiopungua 11 wameuawa katika mji mkuu wa Mali, Bamako na makumi ya wengine wamejeruhiwa kufuatia maandamano yanayoendelea kwa siku kadhaa sasa, yakimtaka Rais wa nchi hiyo Ibrahim Boubacar Keita ajiuzulu.

 

Tags