Uturuki na Misri katika ncha ya kutumbukia kwenye vita nchini Libya
(last modified Sun, 19 Jul 2020 06:39:46 GMT )
Jul 19, 2020 06:39 UTC
  • Uturuki na Misri katika ncha ya kutumbukia kwenye vita nchini Libya

Kushadidi hitilafu za Uturuki na Misri kuhusiana na kadhia ya Libya kumezifanya nchi hizo zipigane makumbo katika Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.

Katika mkondo huo, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan amekosoa hatua ya hivi karibuni za serikali ya Misri na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa jenerali muasi, Khalifa Haftar na kusema kuwa: Nchi yake itaisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya dhidi ya uvamizi wa Misri na kamwe haitawacha peke yao watu wa Libya. 

Alkhamisi iliyopita Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri alidai kuwa majeshi ya nchi yake yataingia katika ardhi ya Libya kwa shabaha ya kulinda usalama wa kitaifa wa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa: "Mji wa Sirte na kambi ya jeshi la anga ya al Jufra nchini Libya ni mstari mwekundu wa Misri ambao haupaswi kuvukwa na upande wowote."

Al Sisi

Itakumbukwa kuwa mwezi Disemba mwaka jana serikali ya Uturuki ilitia saini makubaliano na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya kuhusiana na ushirikiano katika Bahari ya Mediterania na kupanua ushirikiano wa kijeshi na kiusalama wa pande hizo mbili. Kufuatia matukio ya karibuni huko Libya, serikali ya Misri imetuma barua mbili tofauti kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Baraza la Usalama la umoja huo ikipinga rasmi makubaliano hayo. Serikali ya Cairo imesema hatua hiyo ya Ankara na Tripoli inakiuka makubaliano ya Suheirat yaliyotiwa saini nchini Morocco mwaka 2015 baina ya pande zote za Libya kwa shabaha ya kukomesha mgogoro wa ndani na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya. Vilevile Cairo imesisitiza kuwa, makubaliano ya Uturuki na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa yanapingana na maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na kadhia ya Libya likiwemo azimio nambari 1970. 

Baada ya vitisho vya karibuni vya Misri kwamba itavamia ardhi ya Libya, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uturuki, Yashar Yakish, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya nchi hiyo ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na kuwekwa kando nyenzo za kidiplomasia katika mgogoro wa Libya na kusema: Hali ya sasa ya hitilafu baina ya Cairo na Ankara  kuhusiana na Libya yumkini ikasababisha vita baina ya Uturuki na Misri. 

Yashar Yakish: Uturuki na Misri yumkini zitapigana kutokana na mzozo wa Libya.

Pamoja na hayo yote inatupasa kusema hapa kuwa malalamiko hayo ya Misri yametolewa baada ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya kutoa kipigo kikali kwa wapiganaji wa Khalifa Haftar wanaosaidiwa na Misri, Saudi Arabia, Imarati na washirika wao. Ushindi huo umepatikana kwa msaada wa majeshi ya Uturuki yaliyotumwa Libya kuisaidia serikali ya Tripoli. Suala hili limezitia wasiwasi mkubwa nchi hizo zinazomsaidia jenerali muasi Khalifa Haftar. Misri ina wasiwasi kwamba, ushirikiano wa Uturuki na Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake makuu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli utayapa majeshi ya Uturuki fursa ya kuwepo katika eneo hilo la kaskazini mwa Afrika na katika Bahari ya Mediterania. Suala hilo limekuwa tata zaidi baada ya nchi waitifaki wa Haftar yaani Misri, Imarati na Saudi Arabia kushindwa kufikia malengo yao nchini Libya.

Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, kutokana na mgongano wa maslahi baina ya nchi zinazoshiriki katika mgogoro wa Libya, itakuwa vigumu kupatikana ufumbuzi wa mgogoro huo katika siku chache za hivi karibuni.  

Tags