Misri sasa yadai inapinga uingiliaji wowote wa kigeni nchini Libya
(last modified Sat, 25 Jul 2020 07:50:36 GMT )
Jul 25, 2020 07:50 UTC
  • Misri sasa yadai inapinga uingiliaji wowote wa kigeni nchini Libya

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amedai kuwa nchi yake inapinga uingiliaji wowote wa kigeni nchini Libya.

Sameh Shoukry amedai kuwa, Cairo inataka kulindwa mamlaka ya taifa na umoja wa ardhi yote ya Libya. Shoukry amedai pia kwamba Misri inafuatilia kutatuliwa mgogoro wa Libya kwa njia za kisiasa.

Msimamo huo mpya wa Misri kuhusiana na matukio ya Libya umetangazwa na waziri wake wa mambo ya nje wakati bunge la nchi hiyo hivi karibuni lilitoa idhini kwa rais Abdel Fattah el Sisi ya kutuma askari na kujiingiza kijeshi nchini Libya itapolazimu kufanya hivyo; na vilevile likaafikiana na mpango wa kutumwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za kijeshi. 

Kabla ya hapo pia rais el Sisi alisisitiza pia kwamba endapo italazimu, jeshi la nchi hiyo litaingilia mapigano ya kijeshi nchini Libya.

Fayez al-Sarraj (kulia) na Khalifa Haftar

Kwa uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo, Libya ilitumbukia kwenye lindi la mapigano na machafuko na kushuhudia hali ya mchafukoge wa kisiasa, ambapo kwa sasa madaraka ya nchi yamegawika katika pande mbili. Upande mmoja ni wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa (GNA) yenye makao yake katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli. Serikali hiyo inayoongozwa na Fayez al-Sarraj ndiyo inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Na upande mwingine kuna kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar likishirikiana na serikali iliyoko mashariki mwa nchi hiyo katika mji wa Tobruk, ambayo inaungwa mkono na Misri, Saudi Arabia, Imarati na nchi kadhaa za Magharibi.../

Tags