21 Wathibitishwa kufariki katika jengo lililoporomoka Nairobi
Hadi sasa watu 21 wamethibitishwa kupoteza maisha katika jengo lililporomoka kwenye mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Ijumaa.
Kwa mujibu wa waokoaj, watu wengine 135 wameokolewa kutoka katika jengo hilo la ghorofa sita ambalo liliporomoka katika mtaa wa Huruma kufuatia mvua kali mjini humo.
Jitihada za uokoaji zimedorora kutokana na ugumu wa kuingiza vifaa vinavyohitajika katika eneo la jengo hilo ambalo lilikuwa limejengwa karibu na mto.
Wakati huo huo wakaazi wa nyumba za karibu na eneo hilo wametakiwa kuhama kutokana na uwezekano wa kuporomoka nyumba hizo ambazo zimejengwa katika eneo la mto.
Hadi sasa waokoaji wanasema watu 65 hawajulikani waliko na kwamba yamkini wamezikwa katika vifusi vya jengo hilo.
Wawaklishi kutoka mamlaka ya kukagua majengo jijini Nairobi wanasema wanaendesha uchunguzi kuhusiana na walioidhinisha ujenzi wa jengo hilo. Aidha wamesema bado wanaendelea na zoezi la kukagua nyumba kadhaa za ghorofa jijini Nairobi ili kubaini endapo zinafaa kwa matumizi ya makaazi au la.