Kuendelea mivutano juu ya ujenzi wa Bwawa la Renaissance
(last modified Thu, 30 Jul 2020 09:26:43 GMT )
Jul 30, 2020 09:26 UTC
  • Kuendelea mivutano juu ya ujenzi wa Bwawa la Renaissance

Mgogoro ulianzishwa na ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile unachukua mkondo mpya siku baada ya nyingine na kila moja kati ya nchi tatu zinazohusika katika mzozo huo, yaani Misri, Ethiopia na Sudan, zinaendelea kufanya jitihada za kulinda mgao wao wa maji ya mto huo.

Wakati huo huo vitisho vilivyotolewa na Misri vya kuanzisha vita kuhusiana na kadhia hiyo vimezusha wasiwasi mkubwa, suala ambalo limepokewa kwa hisia na misimamo tofauti baina ya viongozi wa Ethiopia na Misri ambao bado wanasisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo.

Katika uwanja huu Rais Abdel Fattah al Sisi amekanusha kutoa vitisho vya kuanzisha vita kuhusiana na mzozo wa Bwawa la Renaissance na kusema: "Kuwa na wasiwasi hakuna maana ya kutoa vitisho. Kwa sasa tunafanya mazungumzo, na mazungumzo yenyewe ni vita vinavyochukua muda mrefu."

Abdel Fattah al Sisi

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile tangu mwaka 2011 umezusha mvutano mkubwa baina ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia. Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini mpaka sasa hayajakuwa na matunda. Sambamba na kushadidi mzozo huo mwezi uliopita nchi hizo tatu zilikutana tena chini ya upatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) na kufikia mapatano kwamba, Ethiopia haitajaza maji kwenye Bwawa na Renaissance kabla ya kufikiwa mapano kamili na ya mwisho. Hata hivyo, kinyume na mapatano hayo, Ethiopia imenza awamu ya kwanza ya kujaza maji ya Nile katika bwawa hilo. 

Hatua hiyo ya Ethiopia imezikasirisha nchi za Sudan na Misri ambazo zimeeleza wasiwasi wao mkubwa na kuitaka Ethiopia itekeleza makubaliano yaliyofikiwa. Kwa upande wake Misri imetangaza kuwa, iwapo hakutafikiwa makubaliano, na Ethiopia ikaendelea mbele ya hatua zake, Cairo itachukua maamuzi mengine. Alaa al Dhawahiri ambaye ni mjumbe katika timu ya mazungumzo ya Misri katika mzozo wa Bwawa la Renaissance amesema: "Kujazwa maji katika Bwawa la Renaissance ni tishio kwa usalama na amani ya kimataifa. Misri inachunguza machaguo tofauti na iwapo hakutafikiwa mapatano baina ya nchi hiyo na Ethiopia na Sudan hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu, Cairo itachukua hatua ya upande mmoja."

Vita vya kugombea vyanzo vya maji ni miongoni mwa mambo yanayoitia wasiwasi dunia ya leo hususan baadhi ya maeneo ya Afrika ambayo yanasumbuliwa na uhaba wa maji na mvua. Kwa sasa hali ya mvutano na wasiwasi inatawala uhusiano wa Misri na Ethiopia kutokana na ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile na kila moja kati ya nchi hizo mbili inamrushia lawama mwenzake. Misri inadai kuwa Ethiopia imechukua hatua ya kwanza ya kujaza maji katika bwawa hilo ili iilazimishe Cairo kuondoka kwenye meza ya mazungumzo na baadaye kuituhumu Misri kuwa haitaki kupatikane ufumbuzi wa kisiasa. Mkabala wake maafisa wa serikali ya Ethiopia wanaamini kuwa, ujenzi wa bwawa hilo na kuanza kujazwa maji ndani yake kuna maslahi kwa nchi zote za kanda hiyo.

Balozi wa Ethiopia nchini Russia anasema: “Kwa sasa kunafanyika mazungumzo ya pande tatu chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika na ninaamini kuwa, matatizo yote yatapatiwa ufumbuzi karibuni. Kwa hakika Bwawa la Renaissance haliwezi kuwa sababu ya vita na mapigano bali litakuwa taasisi muhimu kwa kanda nzima. Bwawa la Renaissance litakuwa chanzo cha ushirikiano na si vita na mizozano.”

Kutokea vita katika eneo hilo la Afrika litakuwa jinamizi kuwa kwa nchi za eneo hilo na dunia nzima hususan katika kipindi cha sasa ambapo Libya ingali inateketea kwa moto wa vita vya ndani huku nchi jirani kama Tunisia, zikiendelea kuzongwa na migogoro ya kisiasa, vitisho vya mashambulizi ya kigaidi, maambukizi ya virusi vya corona na uhaba wa huduma muhimu kama chakula na dawa. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, pande hizo mbili hazina nia ya kuanzisha vita nyingine katika eneo hilo la Afrika licha ya vitisho vya maneno. Kwa msingi huo Misri pia inasisitiza udharura wa kudumishwa mazungumzo licha ya kutishia kutumia nguvu za jeshi kututatua mzozo huo.     

Tags