Wanajeshi wa Marekani wavamia kusini mwa Yemen
Ripoti zinasema kuwa, wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani wamevamia eneo la Kusini mwa Yemen kwa kisingizio cha kuwasaidia wanajeshi wa Imarati katika kile kinachodaiwa ni vita dhidi ya wanamgambo wa al Qaeda katika eneo hilo.
Televisheni ya al-Masirah ya Yemen imedokeza kuwa wanajeshi wao wa Marekani walingia Yemen Aprili 25 kushirikiana na vikosi vya nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia katika hujuma dhidi ya nchi hiyo masikini.
Marekani imetuma wanajeshi Yemen mwaka moja baada ya kuondoa wanajeshi wake nchini humo kutokana na kile ilichosema wakati huo kuwa ni kuzorota hali ya usalama. Magaidi wa al Qaeda nchini Yemen wameimarika katika kipindi cha mwaka moja uliopita tangu Saudia ilipoivamia nchi hiyo ya Kiarabu mwezi Machi 2015.
Hadi sasa watu wasiopungua 9,400 wameshauawa na wengine zaidi ya 16,000 wamejeruhiwa tangu Saudia na washirika wake walipoanzisha mashambulio na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la eti kumrejesha madarakani kibaraka wa utawala wa Aal Saud, Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi. Mashambulio hayo yameangamiza na kusababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya Yemen, mbali na kulenga na kubomoa hospitali, shule, misikiti na turathi za kihistoria za nchi hiyo.