Misri yapinga hatua ya Ethiopia ya kujaza maji katika Bwawa na Renaissance
(last modified Tue, 04 Aug 2020 07:15:49 GMT )
Aug 04, 2020 07:15 UTC
  • Misri yapinga hatua ya Ethiopia ya kujaza maji katika Bwawa na Renaissance

Wizara ya Maji ya Misri imepinga hatua ya upande mmoja ya Ethiopia ya kuanza kujaza maji katika Bwawa na Renaissance.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maji ya Misri imesema kuwa, hatua ya Ethiopia ya kuanza kujaza maji katika bwawa hilo bila ya kushauriana na nchi nyingine za kandokando ya Mto Nile ni ishara kwamba Addis Ababa haina hamu ya kupatikana ufumbuzi wa kiadilifu wa mgogoro huo. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, hatua hiyo ya Ethiopia inapingana na tangazo lililosainiwa mwaka 2015 na nchi tatu za Misri, Ethiopia na Sudan. 

Wizara ya Maji ya Misri imesisitiza udharura wa kuharakishwa mchakato wa kutafuta suluhisho na mwafaka juu ya mgogoro wa Bwawa la Renaissance. 

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance unaofanywa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile tangu mwaka 2011 umezusha mvutano mkubwa baina ya nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia.

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo. Hadi sasa kumefanyika duru kadhaa za mazungumzo baina ya wawakilishi wa nchi hizo tatu lakini mpaka sasa hayajakuwa na matunda. 

Mwezi Juni mwaka huu nchi hizo tatu zilikutana chini ya upatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) na kufikia mapatano kwamba, Ethiopia haitajaza maji kwenye Bwawa na Renaissance kabla ya kufikiwa mapatano kamili na ya mwisho. Hata hivyo, kinyume na mapatano hayo, Ethiopia imenza awamu ya kwanza ya kujaza maji ya Nile katika bwawa hilo.  

Tags