Kushadidi mauaji na ghasia nchini Burundi
Vitendo vya mauaji ya kuvizia nchini Burundi vimezidi kushika kasi nchini humo.
Pierre Nkurikiye, Msemaji wa jeshi la Polisi nchini Burundi amesema kuwa, vitendo vya mauaji ya kuvizia vimeendelea kushika kazi zaidi nchini humo. Nkurikiye ameyasema hayo kufuatia shambulizi lililofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya Christina Nahimana, gavana wa eneo la kaskazini mwa jiji la Bujumbura. Msemaji huyo wa polisi amesema kuwa, licha ya kwamba shambulizi hilo halikusababisha mauaji, lakini limeathiri majengo ya serikali na ya raia katika eneo hilo.
Wiki iliyopita pia Jenerali Athanase Kararuza ambaye pia alikuwa mmoja wa maafisa wa ngazi za juu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi, alishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana, yeye na mke wake. Serikali ya nchi hiyo imetangaza kuwa imewatia mbaroni watu wanne wanaodhaniwa kuhusika na mauaji hayo.
Kufuatia mauaji hayo, Zeid Raad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Masuala ya Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa alinukuliwa akisema kuwa, mauaji dhidi ya viongozi na maafisa wa usalama nchini Burundi, ni jambo ambalo haliwezi kufumbiwa macho. Al-Husseini ametoa wito wa kuanzishwa uchunguzi wa haraka kwa ajili ya kubaini wahusika wa jinai hiyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa kwa mujibu wa ripoti zilizopo, aghlabu ya mashambulizi dhidi ya watu hao yamefanywa na watu wasiojulikana na kwamba, kuongezeka wimbi la vitendo hivyo kunatia wasiwasi mkubwa.
Wakati huo huo Kamishna Mkuu wa Masuala ya Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka serikali na wapinzani nchini Burundi kukaa kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya kurejesha usalama na amani nchini mwao. Hii ni katika hali ambayo, wiki iliyopita kulishadidi vitendo vya ukatili na mauaji ya kuvizia huko Burundi. Mauaji dhidi ya Jenerali Athanase Kararuza na shambulizi la watu wanne wasiojulikana katika soko la Musaga, kusini mwa jiji la Bujumbura ambapo watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa, ni miongoni mwa matukio yaliyoshuhudiwa katika kipindi hicho.
Hivi karibuni Shirikisho la Kimataifa la Muungano wa Mashrika ya Haki za Binaadamu kwa kushirikiana na Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, sanjari na kuelezea ongezeko la mauaji, utesaji na ubakaji ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Burundi, yamelaani pia vitendo hivyo. Mashirika hayo yametangaza kuwa, kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kulipoibuka mgogoro wa Burundi, kumeshuhudiwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu ambao aghlabu umefanywa na maafisa wa usalama wa nchi hiyo na kwa uelewa kamili wa viongozi wa kisiasa.
Muthoni Wanyeki kiongozi wa kieneo wa shirika la Amnesty International amesema kuwa, mauaji, utesaji na kamatakamata ya kiholela ni mambo ambayo yameongezeka sana na kutia wasiwasi mkubwa nchini Burundi. Kufuatia hali hiyo, Jumatatu iliyopita Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Uhalifu ya Umoja wa Mataifa (ICC) alitangaza kuanza uchunguzi wa awali kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Burundi. Uchunguzi huo unaweza kuandaa uwanja wa kuanzishwa uchunguzi mpana zaidi kuhusu mauaji, ukatili na utesaji ambavyo vilianza mwezi Aprili mwaka 2015 nchini Burundi.