Mlipuko watikisa kambi ya jeshi Mogadishu; watu 8 wapoteza maisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62689-mlipuko_watikisa_kambi_ya_jeshi_mogadishu_watu_8_wapoteza_maisha
Mlipuko mkubwa umetokea leo katika kambi ya jeshi huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia na kuuwa watu 8 na kujeruhi wengine 14.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2020 07:11 UTC
  • Mlipuko watikisa kambi ya jeshi Mogadishu; watu 8 wapoteza maisha

Mlipuko mkubwa umetokea leo katika kambi ya jeshi huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia na kuuwa watu 8 na kujeruhi wengine 14.

Halima Abdisalam mwanamama aliyekuwa karibu na eneo la tukio hilo amesema kuwa askari jeshi walifyatua risasi baada ya kutokea mlipuko huo uliosababisha moto mkubwa kutanda angani.

Ameongeza kuwa, watu walikimbia ndani kwa woga na kwamba alishuhudia gari ya jeshi ikienda kwa mwendo kasi na kuwachukua wanajeshi ambao miili yao ilikuwa imejaa damu. “Sijui kama wote wameaga dunia au kujeruhiwa", alisema shahidi huyo.   

Meja Abdullahi Mohamud afisa wa jeshi la Somalia amesema kuwa mlipuko uliotokea leo katika kambi ya jeshi mjini Mogadishu huwenda likawa shambulio la bomu la kutegwa garini.

Mogadishu, Somalia

Habari zinasema kuwa hadi sasa watu 8 wamepoteza maisha na wengine 14 wamejeruhiwa kwenye mlipuko huo. Somalia ilitumbukia katika machafuko makubwa tangu mwaka 1991 wakati wababe wa kivita wa nchi hiyo walipompindua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Mohamed Siad Barre. 

Wakati huo huo kundi la kigaidi la al Shabab limekuwa likifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Somalia tangu mwaka 2008 kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali kuu na kuasisi utawala wake kwa mujibu wa kile kinachotajwa na kundi hilo kuwa sharia za Kiislamu.